OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa Waishukuru USAID-ZAMWASO
HabariHabari Mpya

Mkoa Waishukuru USAID-ZAMWASO

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umelishukuru Shirika la Misaada la Marekani USAID na Jumuia ya Zanzibar Muslim Women AIDS Support Organization (ZAMWASO), kwa msaada wao kwa watoto na kaya zilizo katika hali ngumu kimaisha kutokana na VVU na Ukimwi kwenye Mkoa huo.

Akitoa shukurani hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla amesema Mkoa umefarajika sana na namna USAID na ZAMWASO walivyofanikisha mradi huo wenye lengo la kuwaendeleza watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hayo.

Amesema Mkoa utaendeleza mashirikiano yaliopo baina yake na taasisi hizo ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa na  kueleza  kuwa milango ya Mkoa iko wazi katika kushirikiana na  mashirika na jumuia mbali mbali zenye nia ya kuleta ustawi wa jamii hasa kwa watoto na vijana.

Naye Meneja wa miradi wa ZAMWASO Peter Elias Masoi amesifu mashirikiano makubwa waliyoyapata kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Shehia ambayo yamepelekea kufanikisha  utekelezaji wa programu hiyo na kuiomba Serikali kutenga fedha ili kuendelea kuwasidia watoto na familia zenye hali ngumu kimaisha kutokana VVU na Ukimwi hata baada ya programu hiyo kumalizika.

Amesema jumla ya walengwa 1,772 walifikiwa katika Wilaya ya Mjini kwa mwaka 2021-2022 wakiwemo watoto 240 wanaoishi na maambukizi ya  VVU wamepatiwa misaada mbali mbali kupitia programu hiyo.

Kwa upande wake Bi. Elizabeth Lema kutoka USAID ameeleza kuvutiwa na juhudi zilizochukuliwa na vikundi vya wajasiriamali walionufaika na programu hiyo ambapo waliweza kushiriki kwenye maonyesho mbali mbali ya biashara na kuuza bidhaa zao.

Awali maofisa wa kitengo cha ustawi wa  jamii Mkoa Mjini Magharibi pamoja na watendaji hao kutoka USAID na ZAMWASO walifanya ziara kukagua utekelezaji wa mradi  huo.