OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Wasifu

Mkoa wa Mjini Magharibi ni miongoni mwa Mikoa mitano ya Zanzibar, ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ibara ya 2A ambapo uteuzi wa viongozi na majukumu yao vimebainishwa katika ibara 61 na 62 sambamba na Sheria ya Tawala za Mikoa Namba 8 ya 2014.

Mkoa wa Mjini Magharibi unaongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa na Katibu Tawala Ndugu. Moh‘d Ali Abdallah.


Kiutawala Mkoa wa Mjini Magharibi ni mkusanyiko wa Wilaya tatu; Wilaya ya Mjini, Wilaya ya Magharibi ‘A’ na Wilaya ya Magharibi ‘B’. Mkoa una majimbo 22 ya Uchaguzi, Wilaya ya Mjini majimbo 9 na Wilaya ya Magharibi ‘A’ majimbo 6 na ‘B’ Majimbo 7. Mkoa una wadi 44, Wilaya ya Mjini wadi 18 Magharibi ‘A’ wadi 12 na Magharibi ‘B’ wadi 14. Mkoa una jumla ya Shehia 121, Wilaya ya Mjini ina shehia 56,  Wilaya ya Magharibi ‘A’ ina  shehia 31 na Wilaya ya Magharibi ‘B’ ina shehia  34.

Mkoa una eneo la mraba la km. 224, Wilaya ya Mjini kilomita za mraba 16, Wilaya ya Magharibi ‘A ina kilomita za mraba 100 na Magharibi ‘B’ ina kilomita za mraba 108. Mkoa wa Mjini Magharibi una Mabaraza  matatu ya Manispaa nayo ni Baraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ na Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ .

Mkoa Mjini Magharibi umo katika kitovu cha Makao Mkuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jiji la Zanzibar. Mkoa huu umepakana na Bahari ya Hindi upande wa Magharibi. Mkoa wa Kusini upande wa Mashariki na Mkoa wa Kaskazini upande wa Kaskazini.


Mkoa Mjini Magharibi ni kitovu cha shughuli za kiuchumi kwa Mikoa yote ya Zanzibar kwa vile ina miundombinu ya Bandari, Uwanja wa Ndege na Barabara zinazotoka mikoa ya Kusini na kaskazini kuja katika masoko makuu ya kuuzia na kununulia bidhaa.
Takwimu za Sensa za mwaka 2022 zinaonyesha Mkoa wa Mjini Magharibi una idadi ya watu 893,169.

Majukumu ya Mkoa
Mkoa unatekeleza majukumu ya kila siku kwa mujibu wa Sheria namba 1 ya mwaka 1998 ya Mamlaka ya Tawala za Mikoa ambayo ni pamoja na:

  1. Kuratibu, kufuatilia, kusimamia na kusaidia utekelezaji wa kazi za Serikali pamoja na Shughuli za maendeleo.
  2. Kuhakikisha kuwa, sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa inatekelezwa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
  3. Kuhakikisha kuwa, sera, mipango na maelezo ya serikali yanatekelezwa.
  4. Kuhakikisha kuwa, rasilimali zote kama vile vifaa na nguvu kazi vinatumika kwa maendeleo ya uchumu na ustawi wa jamii.