OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>“Ipo haja kwa Watumishi kupatiwa Mafunzo ya Ulinzi wa Mifumo ya Mitandao” RC Kitwana.
HabariHabari Mpya

“Ipo haja kwa Watumishi kupatiwa Mafunzo ya Ulinzi wa Mifumo ya Mitandao” RC Kitwana.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Idrissa Kitwana Mustafa amesema ipo haja kwa Watumishi kupatiwa Mafunzo ya Ulinzi wa Mifumo ya Kompyuta na kuzuwia wizi wa Mitandao ili waweze kulinda taarifa mbalimbali zilizopo nchini.

Alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mafunzo ya Ulinzi wa Mifumo ya Kompyuta na kuzuwia wizi wa Mitandao (Cyber Security) yanayofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hija katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar.

Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la uwepo wa udukuzi wa tarifa za mtu mmoja mmoja na hata baadhi ya Taasisi jambo ambalo linaweza kusababisha matatizo mengi katika jamii ikiwemo uvunjivu wa Amani.

Alisema endapo Watumishi hasa Wataalamu wa Kompyuta watapata uelewa wa hali ya juu kuhusu mbinu zinazotumiwa na Wahalifu wa Mitandao wataweza kuisaidia Nchi kutunza na kudumisha Amani iliyopo.

Aidha Mkuu wa Mkoa huyo amewasisitiza wale wote watakaopata Mafunzo hayo muhimu, waitumie elimu hiyo katika kuleta maendeleo nchini na kuisaidia jamii kuepuka udhalilishaji unaofanywa Mitandaoni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Taasisi ya Karume, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango Utawala na Rasilimali Watu Dkt.Iddy khatib Iddy amesema miongoni mwa malengo ya Taasisi ya Karume ni kutoa taalum ya mambo yanayoendana na wakati uliopo ikwemo taaluma ya ulinzi wa Mifumo na Komputa.

Alisema kuwa, Mafunzo hayo yatawawezesha Watu binafsi na Taasisi mbalimbali hasa za Serikali, kupata ulinzi wa taarifa zao.

Aidha alitumia fursa hiyo kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na Taasisi ya Karume hasa katika kufanikisha suala la kutumia Mkonga wa Taifa.