OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Kikao cha pamoja kitaondoa changamoto za ukusanyaji wa mapato – Mhe. Kitwana
HabariHabari Mpya

Kikao cha pamoja kitaondoa changamoto za ukusanyaji wa mapato – Mhe. Kitwana

Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi imewafiki ushauri wa  kukaa pamoja na taasisi mbali mbali za Serikali zinazokusanya mapato ili kuweza kuondoa changamoto ziliopo katika ukusanyaji mapato baina ya taasisi hizo na Mabaraza ya Manispaa yaliomo ndani ya Mkoa huo.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha pamoja kilichoshirikisha Uongozi wa Mkoa, Wilaya na Mabaraza ya Manispaa yaliomo katika Mkoa huo pamoja na Uongozi wa Baraza la Usimamizi wa Leseni, kilichofanyika Afisi ya Mkuu wa Mkoa Vuga.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema kwamba suala la kukaa pamoja na taasisi hizo ndio njia pekee itakayoweza kuondoa changamoto ziliopo na kuja na njia bora ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kwa kila taasisi.

Ametahadharisha kuwa iwapo changamoto ziliopo hazitapatiwa ufumbuzi, itafika wakati Mabaraza ya Manispaa hayataweza kufikia malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato kutokana na maeneo mengi yaliyopanga kukusanya kuchukuliwa na taasisi nyengine  za Serikali.

Mkuu wa Mkoa amesema mbali na kuwa Mabaraza ya Manispaa yana  jukumu la kusimamia suala la usafi, vile vile yanawajibu wa kusaidia huduma muhimu za kijamii, vijana na wajasiriamili, kwa hiyo bila ya kuwa na vianzio vya kutosha vya kukusanya mapato, Manispaa hizo hazitaweza kufikia malengo.  

Aidha Mkuu wa Mkoa Amewataka Wakurugenzi wa Mabaraza ya Manispaa kushiriki katika vikao wanavyoalikwa na sekta mbali mbali badala ya kupeleka wawakilishi wao. Amesema ushiriki wao ni muhimu katika utekelezaji wa masuala mbali mbali ya Serikali kuu yanayohusu Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Usimamizi wa Leseni Rashid Ali Salum amesema kwamba Taasisi mbali mbali zimeanzisha vyombo vya ukusanyaji wa mapato katika maeneo ambayo hapo nyuma Mabaraza ya Manispaa yalikuwa yakikusanya mapato, hivyo kikao cha pamoja na taasisi hizo kitaweza kuondoa changamoto ziliopo.

Amesema pia ni vyema kuangaliwa upya sheria na kanuni  zenye mapungufu na kuzifanyia marekebisho ili kuondoa mgongano wa ukusanyaji mapato miongoni mwa taasisi hizo.