OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wasimamizi wa Mradi wa Kijana Nahodha wasisitizwa kuzingatia vigezo.
HabariHabari Mpya

Wasimamizi wa Mradi wa Kijana Nahodha wasisitizwa kuzingatia vigezo.

Katibu Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdallah amewaagiza wasimamizi wa mradi wa Kijana Nahodha kuwa waadilifu pamoja na kuzingatia vigezo katika kuwachagua vijana watakaojiunga na mradi huo.

Ametoa agizo hilo alipokuwa akifungua kikao kazi kwa ajili ya uhamasishaji kuhusu mradi huo kwa Masheha wa Wilaya ya Mjini kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Amani.

Amesema mradi wa Kijana Nahodha unakwenda kuwajengea uwezo vijana waweza kujitegemea kimaisha wakiwemo walemavu, mayatima, waliokatisha masomo, wenye mazingira magumu na makundi mengine maalum, hivyo amesisitiza kuwepo kwa mashirikiano ili lengo la mradi huo liweze kufikiwa.

Aidha amelishukuru Shirika la Misaada la Marekani (USAID), kwa kuja na mradi huo ambao unaenda sambamba na sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwawezesha vijana kujitegemea kwa kuajiajiri wenyewe ama kuajiriwa katika sekta mbali mbali.

Nae mtekelezaji wa mradi huo kwa Zanzibar Bi Samira Seif amesema vijana watakaonufaika na mradi huo wataweza kuendelea na masomo ya sekondari, kujifunza ujasiriamali, mafunzo mbali mbali ya kazi za amali pamoja na kuwashirikisha katika shughuli zitakazowajenga mwili na kiakili.

Aidha amefahamisha kuwa mradi umeanza utekelezaji wake kwa kufanya mikutano na masheha ili kuanza zoezi la kuwaorodhesha vijana watakaoingizwa katika programu hiyo.

Kwa upande wao Masheha wa Wilaya ya Mjini wamesema kuwa mradi huo  utasaidia kupunguza idadi ya vijana wasio na ajira katika Shehia zao. Mradi wa Kijana Nahodha ulizinduliwa rasmi mwezi februari mwaka huu na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi ukiwa na lengo la kuwafikia vijana wa mikoa yote ya Zanzibar na Mikoa mitatu ya Tanzania Bara wenye umri wa miaka 15 hadi 25 chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la watu wa Marekani la USAID.