OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Sherehe za maadhimisho ya miaka 75 ya uhuru wa Pakistani, Zanzibar
Uhuru Pakistan
HabariHabari Mpya

Sherehe za maadhimisho ya miaka 75 ya uhuru wa Pakistani, Zanzibar

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 75 ya uhuru wa Pakistani, Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, alieleza nchi mbili hizo zina historia ya muda mrefu inayotakiwa kuimarishwa.

Alisema viongozi waliotangulia wa nchi mbili hizo, walifanya kazi kubwa kuhakikisha zinakuwa huru hivyo ni julkumu la wananchi na viongozi wa sasa kuimarisha uhuru huo kwa kujenga uchumi imara.

Kitwana alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Pakistani kuja kuwekeza Zanzibar kwa kuwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, imerahisisha mifumo ya uwekezaji kuvutia wawekezaji katika Nyanja mbali mba;li za kiuchumi na kijamii.

Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Pakistan – Zanzibar

“Zanzibar ina mwingiliano mkubwa na watu wenye asili ya Pakistani, hivyo nawaomba nyinyi wenyewe mliopo hapa au ndugu zetu waliopo Pakistani, kutumia fursa kuwekeza miradi itakayoimarisha uchumi wenu na mataifa yetu kwa ujumla,” alieleza Kitwana.

 Aidha aliwapongeza viongozi, wananchi na wana Jumuiya ya Wapakistani wanaoishi Zanzibar kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa nchi yao akieleza kuwa pia ni furaha ya wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Balozi mdogo wa Pakistani nchini Tanzania, Muhammad Azan Bihan, alieleza kufurahishwa kwake na jinsi nchi yake na Tanzania zinazovyoendeleza uhusiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 75 ya uhuru wake, Pakistani imepiga hatua mbali mbali za kimaendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa jambo linalotoa fursa kwa wananchi wake kujiendeleza.

 Akisoma ujumbe wa Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Balozi Bihan alieleza hatua mbali mbali ambazo nchi hiyo imechukua katika kuimarisha ustawi wa jamii na uchumi wa Pakistani.

Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Pakistan – Zanzibar

Alisema kwa wakati tofauti serikali ya nchi hiyo imefanya mapitio ya sera na mifumo ya kiuchumi jambo lililochangia ukuaji wa kasi ya uchumi wa nchi hiyo hususan katika sekta ya kilimo, teknolojia na maendeleo ya jamii.

Aidha Balozi Bihan aliwanukuu viongozi hao wakisema pamoja na kuzuka kwa janga la maradhi ya corona, nchi hiyo imeelea kupiga hatua huku ikiendeleza mikakati ya kupambana na janga hilo kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa.

Kuhusu maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Balozi huyo alipongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali zote mbili za Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya kiuchumi lakini pia hali ya amani na utulivu.

Alisema hali hiyo ni kivutio kikubwa kwa ukuaji wa uchumi na kuahidi kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kuongeza tija katika uchumi.

Awali akizungumza katika sherehe hizo zilizofanyika katika hoteli ya Marumaru, Shangani Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wapakistani waishio Zanzibar, Muhammad Abid Abubakar, alieleza kuwa lengo la jumuiya hiyo ni kuwaunganisha wapakistani waliopo Zanzibar ili waendelee kututumia fursa ziliopo Zanzibar na nchini kwao.

Alisema kupitia jumuiya hiyo, watahakikisha wananchi wa Zanzibar wananufaika na fursa zitakazokuwa zinazotolewa na serikali ya Pakistani ili kuchangia maendeleo ya watu wake.

“Kwa kipindi kirefu raia wa Pakistani na Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa furaha na maelewano lakini pia watu wa jamii nyengine jambo linalotuwezesha kufanya shughuli zetu bila ya bughudha,” alieleza Abid.

Pakistani inayopatikana katika bara la asia, ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1947 hatua iliyoliwezesha taifa hilo kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mengine ikiwemo Tanzania mnamo mwaka 1967 ambapo Pakistani ilifungua ofisi za Ubalozi nchini.