OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Ujenzi wa skuli ya Muungano akabidhiwa  mkandarasi
HabariHabari Mpya

Ujenzi wa skuli ya Muungano akabidhiwa  mkandarasi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kujenga miundombinu bora ya majengo ya Skuli ili kuboresha huduma za elimu nchini.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali  Mhe. Lela Mohammed Mussa amesema hayo katika hafla ya utiaji saini ya mkataba na kukabidhi kazi ya  ujenzi kwa kampuni ya FUCHS, hapo Skuli ya Muungano.

Amewataka wakandarasi  kuhakikisha wanajenga Skuli yenye ubora na kiwango cha hali ya juu pamoja na kumaliza kwa wakati  kwa kuzingatia makubaliano ya mkataba huku akisisitiza umuhimu wa  kuwapatia nafasi za kazi  vijana wazalendo katika ujenzi wa mradi huo.

Akitoa ufafanuzi juu ya wanafunzi wanaosoma Skuli hiyo ya Muungano, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa  amesema baadhi ya wanafunzi watahamishiwa kwa muda katika Skuli ya Sebleni na wanafunzi wengine watasoma katika Skuli ambazo zipo karibu na makaazi yao .

Amesema kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi, Skuli hiyo yenye madarasa 13 itavunjwa na kujengwa  yenye madarasa 41  ili kukidhi mahitaji pamoja na kupunguza tatizo la  wanafunzi wa eneo hilo kufuata masomo Skuli za mbali .

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Muungano Ali Maulidi  amesema skuli hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi ambapo darasa moja lina  zaida ya wanafunzi 100 jambo ambalo linashusha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi, Hivyo ameishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Elimu kwa uamuzi wao wa kujenga Skuli hiyo.  

Skuli hiyo ya ghorofa tatu itakapo kamilika  itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafumzi 1,845 na  inatarajiwa kuanza ujenzi wake April 2023  na kumalizika Novemba 2024 ikiwa  ni mojawapo ya Skuli 21 zitakazojengwa  Zanzibar.