OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa watakiwa kudhibiti ombaomba
HabariHabari Mpya

Mkoa watakiwa kudhibiti ombaomba

Kamati ya kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ya Baraza la Wawakilishi imeutaka uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na ongezeko la omba omba katika Mkoa huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Machano  Othman Said amesema  Kamati yake hairidhishwi na hali hiyo ambayo imekuwa ikionekana kuongezeka siku hadi siku.

Akizungumza na uongozi wa Mkoa huo katika ukumbi wa mikutano Afisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, amesema kutokana na ukarimu wa watu wa Zanzibar baadhi  ya watu  wamekuwa wakitumia  sababu za  ulemavu  kuwa omba omba hali ambayo haileti sura nzuri katika maeneo mbali mbali ya Mji.

Aidha Mhe. Machano ameupongeza Mkoa wa Mjini Magharibi kwa jitihada kubwa wanazochukua katika  kudumisha ulinzi na usalama katika Mkoa huo na kusema kuwa hali hiyo imezidi  kuimarika kwasasa.

Kwa upande mwengine ameyataka Mabaraza ya Manispaa Mjini, Magharibi A na B kuongeza juhudi katika suala la usafi ili kuenda sambamba na ujenzi wa  miundombinu ya  barabara zinazoendelea kujengwa katika Mkoa huo.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mtumwa Peya Yussuf ameeleza licha ya hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali kupambana na vitendo vya udhalilishaji bado vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka kwa kasi, hivyo ameutaka Mkoa kulichukulia hatua zaidi suala hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Kamati  likiwemo suala la udhalilishaji, omba omba, usafi wa mji, ulinzi pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wake.

Awali Kamati ya Viongozi Wakuu wa Serikali ilipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mkoa Mjini Magharibi kwa kipindi cha Januari hadi  Machi 2023.