OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wafanyakazi wa Umma watakiwa kutoa mashirikiano kwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar
HabariHabari Mpya

Wafanyakazi wa Umma watakiwa kutoa mashirikiano kwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar

Wafanyakazi wa umma wametakiwa kutoa mashirikiano yao kwa  Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF),  ili mfuko huo uweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugnzi Mkuu wa ZHSF  Yassir Ameir Juma kwenye kikao chake na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi kuzungumzia masuala mbali mbali juu ya mfuko huo .

Akizungumza  katika kikao hicho  kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hapo Vuga, Yassir amefahamisha kuwa tarehe 20 mwezi huu ndio itakuwa tarahe ya mwisho ya usajili wa wafanyakazi wa  umma,  hivyo amewataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kukamilisha usajili  wao kabla ya tarehe hiyo.

Ameongeza kuwa ZHSF  itaanza rasmi kutoa huduma  kwa wanachama wake kuanzia mwezi wa  Octoba 2023 katika vituo vya afya na Hospitali mbali mbali katika Mikoa yote ya Zanzibar.

Aidha amesema kwamba Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar  unaendelea na mazungumzo na taasisi husika ili kuona wanachama wa mfuko huo wanaweza kutumia  kadi zao kupata matibabu katika hospitali za  Tanzania bara.

Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza pia  ZHSF itakuwa ikifanya zoezi la ufuatiliaji  na kukagua huduma zinazotolewa katika vituo vya afya na Hospitali ili kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma bora.

Amewaeleza wafanyakazi hao kuwa dhamira ya Serekali  kuanzisha mfuko huo ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Zanzibar wanapata huduma bora za afya pamoja na kuwapunguzia mzigo wa kutumia gharama kubwa kulipia matibabu pale wanapopata maradhi mbali mbali.

Naye Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdallah amewataka wafanyakazi hao kuitumia taaluma walioipata kwa kuwaelimisha wafanyakazi wenzao wa umma kuhusu mfuko huo.

Kwa upande wao wafanyakazi wa Ofisi hiyo wameuomba uongozi  wa  ZHSF kuhakikisha kuwa huduma zitakazotolewa katika hospitali ambazo watakuwa wakipatiwa matibabu zinakuwa bora kwa upande wa madaktari, vipimo na madawa.