OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Masheha kutoa maoni juu ya Kanuni ya Makaazi ya Watalii
HabariHabari Mpya

Masheha kutoa maoni juu ya Kanuni ya Makaazi ya Watalii

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema uwepo wa Kanuni ya Makaazi ya Watalii kutasaidia kuthibiti  matumizi ya nyumba zinazolaza wageni kwenye Shehia.

Amesema hayo wakati akifungua mkutano wa kupokea maoni ya Masheha wa Mkoa Mjini Magharibi kuhusu Kanuni ya Makaazi ya Watalii uliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni.

Amesema kwamba Masheha kama viongozi wa Serikali ngazi ya  shehia  wanafahamu hali halisi ilivyo  katika Shehia zao hivyo uamuzi wa Kamisheni ya Utalii kupokea maoni yao  kutasaidia kuiboresha kanuni hiyo.

Mkuu wa Mkoa  ameihakikishia Kamisheni ya Utalii kuwa Mkoa utatoa kila aina na mashirikiano ili kuona  kanuni hiyo inasimamiwa ipasavyo ndani ya Mkoa wake.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa aliwataka Masheha kutoa maoni yao yatakayosaidia kuiboresha Kanuni hiyo.

Amesema kwamba zipo nyumba katika Shehia zao zinazotumika kulaza wageni bila kufuata sheria na kupelekea kuikosesha mapato Serikali, hivyo aliwataka Masheha kuzitambua nyumba hizo pamoja na wageni wanaoingia.

Akiwasilisha Kununi ya Makaazi ya Watalii mwanasheria kutoka Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Mustafa Omar Abdalla amesema Serikali imeamua kuweka kanuni hiyo ili nyumba hizo zifanye biashara kwa mujibu wa taratibu na kuiwezesha Serikali kuingiza kipato.

Vilevile amesema kanuni hiyo imewekwa kwa makusudi  ili kuona nyumba zinazolaza watalii zinakidhi sifa na kuhakikisha usalama wa wageni hao.