OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC Kitwana asisitiza ubora wa miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru
RC kitwana
HabariHabari Mpya

RC Kitwana asisitiza ubora wa miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa miradi yote itakayozinduliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kukaguliwa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru inatimiza sifa na vigezo vinavyotakiwa.

Agizo hilo amelitoa wakati Kamati ya Usalama ya Mkoa Mjini Magharibi ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa ilipofanya ziara katika Wilaya ya Mjini, Magharibi “A” na Magharibi “B”  kukagua miradi itakayotembelewa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Akijibu maswali ya Waandaishi wa Habari, Mkuu wa Mkoa amesema, Kamati ya Usalama inatakiwa kujiridhisha ili kuhakikisha miradi yote imetimiza vigezo vitakavyopelekea Mwenge wa Uhuru kufika kwenye miradi hiyo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya kuzifanyia kazi kasoro ndogo ndogo zilizobainika wakati wa ziara hiyo kabla Mwenge wa Uhuru haujaanza Mbio zake kwenye Wilaya zao.

Wakati huo huo Idrissa ametoa wito kwa Taasisi za Serikali, binafsi, wafanyabiashara na wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuchangia Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Ameeleza kwamba fedha zitakazopatikana zitakwenda kuongeza nguvu katika miradi inayowagusa wananchi ikiwemo ya wajasiriamali, hivyo amewataka kuwa na moyo wa kuchangia Mwenge wa Uhuru.

Ameongeza pia Mkoa wake umejipanga vizuri ili kuona safari hii wanapata ushindi kati  ya moja ya Wilaya zake kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu.

Naye Kaimu Kamanda wa Polisi  Mkoa Mjini Magharibi Elisante Mmari  amesema kwamba wamejipanga vizuri kuhusu suala la ulinzi katika maeneo yote Mwenge wa Uhuru utakapopita ndani ya Mkoa huo.

Mwenge wa Uhuru utaanza Mbio zake  Mkoa Mjini Magharibi tarehe 23 Mei ukitokea Mkoa wa Kusini Unguja.