OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa wapata mafanikio utekelezaji wa Ilani ya CCM
HabariHabari Mpya

Mkoa wapata mafanikio utekelezaji wa Ilani ya CCM

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umeeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zaznibar imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2020-2025 ndani ya Mkoa huo.

Hayo yamesemwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa Mjini Kichama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akizungumza na Katibu mpya wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mjini Kichama Innocent Nyanzaba alipofika Afisini kwake Vuga kujitambulisha.

Amesema ndani ya kipindi cha miaka miwili cha Serikali ya awamu ya nane miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbali mbali imejengwa katika Mkoa Mjini Magharibi huku miundo mbinu mingine ikiwemo majengo ya Skuli ,masoko na barabara  ujenzi wake ukiendelea kutekelezwa kwa kasi.

Amemueleza Katibu huyo kuwa Serikali ya Mkoa inaendelea kufatilia utekelezaji wa ilani ya CCM ili kuhakikisha yale yote yaliyokusudiwa kutekelezwa ndani ya Mkoa huo  yanakamilika kabla ya mwaka 2025.

Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amemueleza Katibu huyo kuwa, Serikali ya Mkoa itampa kila aina ya mashirikiano katika kutekeleza majukumu yake ndani ya Mkoa huo.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mjini Kichama Innocent Nyanzaba amesema kuwa  Serikali iliyopo madarakani inatekeleza ilani ya CCM,  hivyo kila mfanyakazi anawajibu wa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa ilani inavyoelekeza.

Aidha ameahidi  kuendeleza mashirikiano yaliopo baina ya Serikali na Chama cha Mapinduzi  katika utekelezaji wa masuala mbali mbali yenye lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.

Nae Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Mjini Kichama Salama Abasi Juma amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa mabadiliko hayo ya uongozi yanakwenda kuimarisha zaidi utendeji wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya Mkoa.

Mkoa Mjini Magharibi una jumla ya majimbo 9 na wadi 18 ambayo yote yanashikiliwa na Chama cha Mapinduzi.