OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Bilioni 40 kutumika kwa ujenzi  wa Skuli
HabariHabari Mpya

Bilioni 40 kutumika kwa ujenzi  wa Skuli

Zaidi ya shilingi bilioni arubaini zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi  wa Skuli saba za horofa zinazoendelea kujengwa maeneo mbali mbali katika Mkoa Mjini Magharibi.

Akikagua ujezi wa Skuli ya ghorofa tatu ya Muungano katika Wilaya ya Mjini, Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla ameitaka Kampuni ya  Fuch Construction inayojenga Skuli hizo  kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati ili  kuleta tija  kwa wananchi pamoja kutimiza malengo   yaliyokusudiwa na Serikali.  

Amewaeleza wasimamizi wa mradi huo kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa Skuli hizo na ipo tayari kutoa kila aina ya msaada utakaohitajika ili kuona changamoto yoyote itakayojitokeza inapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Katibu Tawala amesema kwamba ujenzi wa majengo hayo unaoendelea kwa kasi  katika Mkoa wake utaleta faida kubwa kwa upande wa sekta ya elimu kwavile utapunguza idadi ya wanafunzi madarasani pamoja na kutoa nafasi  zaidi za ajira ya walimu.

Sambamba na hilo ameeleza matumaini yake kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaweza kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa ngazi ya msingi na Sekondari na kuinua kiwango cha elimu katika Mkoa huo.

Katibu Moh’d amewataka wananchi wa Mkoa huo kuunga mkono jitihada  zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa kwenye Mkoa Mjini Magharibi ikiwemo  sekta ya elimu barabara na miundo mbinu mengineyo.

Akizungumzia mradi huo Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Fuchs Contraction kutoka Tanzania Bara Ali Khamis Omar amesema jumla ya Skuli tano za horofa tatu na Skuli tatu za horofa mbili zinaendelea kujengwa na Kampuni yake saba zikiwa katika Mkoa Mjini Magharibi na moja Mkoa kusini Unguja.

Ameeleza kuwa kazi ya ujenzi wa Skuli hizo inaendelea vizuri licha ya changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza hapo awali kutokana na mvua za masika na wanatarajia kukamilisha mradi huo mwezi Disemba mwaka 2023.

Afisa uhusiano huyo amezitaja Skuli zilizonufaika na mradi huo katika Mkoa Mjini Magharibi ni Chukwani, Muungano, Chumbuni, Regeza Mwendo, Mwera, Kijichi na Maungani.

Aidha ameziomba taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na mradi huo kuwapa mashirikiano ili waweze kukamilisha kazi hiyo kwa wakati waliyokusudia.

Wakati huo huo Katibu Tawala alikagua ujenzi wa Skuli ya horofa mbili ya Mwembeladu inayojengwa na Kampuni CRJE ya China yenye madarasa 45 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 95 na inatarajiwa kuamilika mwezi ujao.