OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC Kitwana azindua Kampeni ya Kata Bima bila Shuruti
HabariHabari Mpya

RC Kitwana azindua Kampeni ya Kata Bima bila Shuruti

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amezindua Kampeni ya “Kata Bima Bila Shuruti” yenye lengo la kukakikisha vyombo vyote vya moto vinavyotembea barabarani vimekatiwa bima.

Amesema kampeni hiyo itakayosimamiwa na Askari wa Usalama barabarani kwa kushirikiana na Askari wa Vikosi vya SMZ itafanyika katika Wilaya zote tatu za Mkoa Mjini Magharibi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mkoa Mjini Magharibi katika uzinduzi huo uliofanyika Uwanja wa Mnazi Mmoja kikwajuni, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka amekitaka kikosi kinachosimamia zoezi hilo kutokuwa na muhali dhidi ya madereva watakaowakamata kuendesha vyombo  visivyo na bima na kuwataka  kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesema Mkoa unaunga mkono Kampeni hiyo iliyoanzishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA),Tawi la Zanzibar na kutoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya moto kuvikatia bima vyombo vyao ili kuepuka usumbufu.

Aidha Mkuu wa Mkoa amesema zoezi hilo la ukaguzi wa bima litafanyika kwa vyombo vya Serikali , hivyo amewataka viongozi wa taasisi mbali mbali za umma hukakisha vyombo vyote vya taasisi zao vina bima pale vinapotembea barabarani.

Amesisitiza kuwa bima ya gari na vyombo vyengine vya moto ina umuhimu mkubwa kwa vile itawezesha waathirika kulipwa fidia wakati wanapopata ajali pamoja na kuiwezesha  Serikali kukusanya mapato yake.

Mkuu huyo wa Mkoa ameelea pia  Askari watakaosimamia Kampeni hiyo wamepewa mafunzo kuhusiana na masuala ya bima na namna ya kuwachukulia hatua madereva watakaowakamata  ili kampeni hiyo iweze kufanyika kwa ufanisi.

Ameipongeza TIRA kwa kuja na Kampeni hiyo ambayo imeanza katika Mkoa wake na kuahidi kutoa kila aina ya mashirikianao ili lengo liliokusudiwa liweze kufikiwa.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), tawi la Zanzibar Mohammed Khamis Ameir amesema kuwa  wameamua kuja na Kampeni  hiyo kutokana na wahanga wengi wa ajali za barabarani hawawezi kulipwa fidia na hivyo kuingia hasara   kutokana na vyombo vyao kutokatiwa na bima.

Amefahamisha kuwa suala la bima sio la hiari  bali ni la lazima kwa mujibu wa sheria ambapo chombo chochote cha moto kinachotembea barabarani kinatakiwa kiwe kimekatiwa bima angalau daraja la tatu.

Mara tu baada ya uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Mjini aliongoza Kampeni hiyo ambapo zaidi ya gari na vyombo vya maringi mawili 30  vizivyo na bima vilikamatwa.