OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC Kitwana ameushauri Uongozi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere kutambua mipaka ya eneo lao
HabariHabari Mpya

RC Kitwana ameushauri Uongozi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere kutambua mipaka ya eneo lao

 Uongozi wa Mkoa wa Mjini  Magharibi umekishauri  Chuo cha  Kumbukumbu  ya Mwalimu  Nyerere kuitambua mipaka  iliyowekwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Maakazi kwenye eneo  lao   huko  Chuini Ngalawa    hadi  pale Serekali itakapotoa maamuzi  kuhusu sehemu wanayoidai inayotumiwa  na waanika dagaa katika eneo hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana  Mustafa  wakati aliponya ziara katika eneo hilo pamoja na uongozi wa chuo hicho, Wizara ya Ardhi,  Wilaya ya Magharibi A na Baraza la Manaispaa.

Akizungumza mara baada ya kukagua eneo hilo na kupata maelezo kutoka Uongozi wa Wizara ya Ardhi, amesema Serikali ya Mkoa itashirikiana na  Wizara ya Ardhi kuhakikisha inalipatia ufumbuzi suala hilo ndani ya muda mfupi.

Amesema kwamba hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Ardhi ya kulipunguza eneo la chuo hicho kwa ajili ya waanika Dagaa litafikishwa Serikalini ili kuangalia namna itakavyofikia maamuzi yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Kwa upande mwengine Idrissa amekitaka chuo hicho kulidhibiti eneo walilopewa na Serikali ili kuepusha uvamizi na matumizi mengine ya wananchi ndani ya eneo lao.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ameiagiza Wilaya ya Magharibi A na Baraza la Manispaa Magharibi A kuwaondoa waanika Dagaa walioingia ndani ya mpaka wa eneo la chuo hicho. Amesema lazima mipaka ya iliyowekwa iheshimiwe ili eneo hilo libaki salama kwa matumizi endelevu ya chuo

Aidha  Mkuu wa Mkoa ameushukuru uongozi wa Wizara ya Ardhi kwa mashirikiano yao makubwa waliyoyatoa katika kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Akitoa maelezo yake kuhusu eneo hilo Naibu Katibu Mkuu Wiara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mzee Haji Ali amesema kwamba  Serikali imelipunguza eneo la chuo hicho hekta 3.8 mwaka 2020 kwa ajili ya waanika Dagaa. Ameongeza kuwa awali chuo hicho kilikua na eneo lenye ukubwa wa hekta 33.1 na baada ya kupunguzwa imebakiwa na hekta 29.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Susan Kunambi ameahidi kulitekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kuwaondoa waanika Dagaa waliongia ndani ya mpaka wa Chuo.

Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Nyerere Tawi la Zanzibar Dkt. Rose Mbwete amesema kwamba kufuatia ziara hiyo anaamini kuwa Serikali itafikia maamuzi yake juu ya mgogoro huo.

Ziara hiyo inafuatia agizo la Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alilolitoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa mabweni ya chuo hicho ambapo aliutaka uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi pamoja na Wizara ya Ardhi kulipatia ufumbuzi suala hilo.