OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wananchi wa Mjini Magharibi wampongeza Dk Mwinyi
HabariHabari Mpya

Wananchi wa Mjini Magharibi wampongeza Dk Mwinyi

Wananchi  wa Mkoa Mjini Magharibi wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo  kwenye Mkoa huo ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.

Pongezi hizo wamezitoa wakati  maofisa habari wa Mkoa na Wilaya za Mkoa  Mjini Magharibi walipozungumza na wananchi mbali mbali kwenye ziara ya kukagua maendelo ya ujenzi wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mjini, Magaribi A na Magharibi B.

Wamesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Nane wameshuhudia   miradi mikubwa ya maendeleo ikitekelezwa kwa kasi katika sekta ya afya, elimu, maji, barabara, majengo ya wajasiriamali na huduma nyengine za kijamii.

Wananchi hao wamesema kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta  manufaa makubwa kwao kwani kutaweza kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu kwenye Wilaya zao.

“Tunamshukuru sana Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa maendeleo makubwa anayotuletea yeye pamoja na Serikali yake, miradi hii itakwenda kutuondoshea shida sisi pamoja na watoto wetu kufuata mbali skuli na huduma za afya.” Alisema Bi. Fatma Ali wa Mbuzini

Aidha wamasema vile vile Serikali imeweza kuviinua vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba pamoja na vitendea kazi zikiwemo boti za uvuvi kwa wavuvi na kinamama wanaojishuglisha na uvuvi wa mwani.

Wamesema hatua hiyo imewasaidi wananchi wa mkoa huo hasa vijana na kinamama kuweza kuendeleza vikundi vyao pamoja na kuinua kipato chao cha maisha kupitia biashara na miradi mbali mbali midogo midogo waliyokwisha ianzisha.

Wamesema kwamba wanathamini sana juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi na wamuomba endelee na kasi hiyo hiyo na kutovunjika moyo na watu wanaobeza mafanikio yaliyopatikana.

Kwa upande mwengine Kampuni iliyopewa kazi ya ujenzi wa miradi ya Skuli za horofa mbili za msingi  ya Mwanakwerekwe na Kwa Binti Amrani wamesifu maamuzi yaliyochukuliwa na Serikali ya ujenzi wa miradi hiyo mikubwa.

“Miradi  hii ni wa mfano kwa shule za msingi ina  vyumba vya komputa, maabara, maktaba na ukumbi mkubwa. Utaweza kuwajenga wanafunzi wa ngazi ya msingi kujifunza mapema kwa vitendo masomo ya sayansi, komputa na kutumia maktaba kwa kujisomea” alisema mhandisi wa Kampuni ya ESTIM inayojenga Skuli hizo Emmanuel William.

Naye Msimamizi wa Kampuni iliyosanifu ramani ya Hospitali ya Mkoa Mjini Magharibi iliyopo Lumumba ndugu  Ramadhan China amesema ujenzi wa Hospitali hiyo ya horofa sita ni moja ya mradi mkubwa kuwahi kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema jengo hilo limesanifiwa kuweza kutoa matibabu ya maradhi mbali mbali na hivyo kuwaondoshea shida wazanzibari kufuata matibabu Tanzania bara na nje ya nchi.

Wakati huo huo  Kampuni zinazojenga miradi mikubwa ya Maji katika Wilaya ya Magharibi A na B wamesema  kazi ya ujenzi wa miradi hiyo imefikia hatua kubwa ambapo tayari wameanza kufanya majaribio ya matangi ya kuhifadhia maji na wanasubiri baadhi ya vifaa viwasili nchini ili kukamilisha kazi iliyobaki. Ujenzi wa miradi ya hospitali, skuli, barabara, maji, majengo ya wajasiriamali ipo katika hatua ya mwisho na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.