OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umesema utashirikiana na Sekta husika ili kupata maeneo yatakayojengwa madarasa yaliyobakia
HabariHabari Mpya

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umesema utashirikiana na Sekta husika ili kupata maeneo yatakayojengwa madarasa yaliyobakia

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umesema kuwa utashirikiana na Sekta husika ili kupata maeneo yatakayojengwa madarasa yaliyobakia katika Mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa wakati Makamu wa Pili wa Rais akikagua ujenzi wa madarasa kwenye Skuli tofauti ndani ya Wilaya ya Magharibi B. Amesema kuwa changamoto ya ukosefu wa maeneo itapatiwa ufumbuzi ili madarasa yote 54 yaliyopangwa kujengwa katika Mkoa Mjini Magharibi kupitia fedha za UVIKO 19 yaweze kujengwa kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohammed Mussa amesema kuwa ujenzi wa madarasa hayo utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wanafunzi kwenye Skuli mbali mbali. Akizungumzia kuhusu ujenzi wa miradi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis amesema wananchi wa Wilaya yake wamekuwa wakitoa mashirikiano makubwa katika ujenzi wa miradi hasa baada ya kutambua manufaa watakayoyapata pale itakapoanza kutoa huduma.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa Magharibi Mohammed Rajab ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa miradi mingi ya maendeleo kwa fedha za UVIKO 19 ndani ya Mkoa wake. Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alitembelea pia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Magharibi B, majengo ya wajasiriamali na Kituo cha Mafunzo ya Amali Bweleo.