OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Serikali haipo tayari kuona miradi ya maendeleo inayojengwa kupitia fedha za UVIKO-19 inacheleweshwa – Mhe. Hemed
HabariHabari Mpya

Serikali haipo tayari kuona miradi ya maendeleo inayojengwa kupitia fedha za UVIKO-19 inacheleweshwa – Mhe. Hemed

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla amesema Serikali haiko tayari kuona miradi ya maendeleo inayojengwa kwa fedha za UVIKO 19 inachelewa kumalizika kwa visingizio mbali mbali. Onyo hili amelitoa huko Mbuzini wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi mbali mbali katika Wilaya ya Magharibi A.

Amesema fedha za ujenzi wa miradi hiyo zipo, hiyo hakuna sababu ya kuchelewa kukamilika kwa miradi yote iliyopanga kutekelezwa na Serikali. Amezitaka sekta zinazosimamia miradi ikiwemo Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya kupeleka maombi ya fedha Wizara ya Fedha na Mipago kwa wakati ili waweze kuingiziwa fedha za kuendeleza ujenzi.

Amewaambia Wakandarasi waliopewa kazi hiyo kuwa Serikali inaamini watamaliza kazi kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wananchi. Akizungumzia kuhusu ujenzi wa madarasa yanayojengwa kwenye Shehia tofauti ndani ya Wilaya hiyo, Makamu wa Pili wa Rais amekipongeza Kikosi cha Kujenga Uchumi JKU kwa kazi nzuri na inayoenda kwa kasi.

Aidha ameipongeza pia Wizara ya Afya kwa kuendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu ujenzi hospitali za Wilaya. Nao wakandarasi wanaojenga miradi hiyo wamemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais kuwa miradi hiyo itakamilika kwa wakati licha ya changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza.