OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wajumbe wataka umakini miradi ya maendeleo Mjini Magharibi
HabariHabari Mpya

Wajumbe wataka umakini miradi ya maendeleo Mjini Magharibi

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kupitia sekta mbali mbali katika mkoa wa Mjini Magharibi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, alieleza hayo katika hutuba aliyoitoa katika mkutano wa kamati ya maendeleo ya mkoa huo uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil 30/01/2022.

Mkutano huo wa kwanza kwa mwaka huu, uliwashirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na wakuyrugenzi za manispaa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na wengine wa serikali na taasisi zisizo za kiserikali.

Alifahamisha kuwa serikali kupitia sekta hizo, imesaini mikataba ya ujenzi kwa baadhi ya miradi ikiwemo miradi ya ujenzi wa hospitali mpya ya mkoa inayojengwa katika eneo la Lumumba kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 24.717.

Alieongeza kuwa ambapo ujenzi wa hospitali 3 za wilaya utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 13.749 ambazo zitajengwa katika maeneo ya Chumbuni kwa wilaya ya Mjini, Magogoni wilaya ya Magharibi ‘B’na Mbuzini kwa wilaya ya Magharibi ‘A’.

“Miradi mengine mikubwa inayoendelea kutekelezwa katika mkoa wetu ni ujenzi wa masoko ya kisasa yanayojengwa Chumbuni ambalo litagharimu shilingi bilioni 46, ujenzi wa soko la Mwanakwerekwe utagharimu shilingi bilioni 39.6 na soko la Jumbi utagharimu shilingi bilioni 17.1 na kwamba ujenzi wa masoko hayo utakapokamilika utasaidia kuongeza nafasi za ajira sambamba na kuimarisha mazingira mazuri ya kibiashara,” alieleza Kitwana.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa serikali ya mkoa itahakikisha inaifuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ikamilike kwa wakati na viwango vinavyokubalika ili kuleta tija kwa wananchi wa mkoa huo na serikali kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusu hali ya usafi wa mazingira katika mkoa huo, Kiwana alieleza kuwa baraza la manispaa limefunga mkataba na kampuni ya Vigor kwa ajili ya ukusanyaji wa taka na kwamba hali ya usafi wa mazingira imeanza kuridhisha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo

Akiwasilisha taarifa ya hali ya ulinzi na usalama kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2021, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Abdallah Hussein Mussa, alisema katika kipindi hicho hali ya ulinzi na usalama imeimarika na kupelekea kupungua kwa makosa ya kihalifu.

Alieleza kuwa katika kipindi hicho, makosa 555 yaliripotiwa ikilinganishwa na makosa 738 yaliyoripotiwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2020 ambapo kuna upungufu wa makosa 183 sawa na asilimia 48 .

Alifahamisha kuwa makosa yanayoripotiwa mara kwa mara ni makosa ya maadili, makosa ya kuwania mali pamoja na dawa za kulevya.

“Makosa ya vitendo vya udhalilishaji yaliyoripotiwa kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2021 yalikuwa ni 228 ambapo kipindi katika kipindi kama hicho mwaka 2020 kesi 215 ziliripotiwa na kupelekea ongezeko la makosa 13 sawa na asilimia 5.70,” alisema ACP Hussein.

Akizungumzia ajali za barabarani kamanda Hussein alieleza kuwa katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2021 ajali za barabarani ni 3,329 ziliripotiwa ikilinganishwa na makosa 4,026 yaliyoriporiwa kwa kipindi kama hicho 2020 ambayo ni upungufu wa makosa 697 sawa na asilimia 17.31

Nae Masoud Omar Masoud, kutoka Wizara ya Elimu Mafunzo ya Amali, alieleze kuwa sekta hiyo imepata mafanikio makubwa hasa katika kuimarisha miundombinu ya sekya hiyo, uandikishaji wa wanafunzi kwa skuli za msingi pamoja na ufaulu wa wa wanafunzi kwa skuli za sekondari.

Aidha liongeza kuwa serikali inatarajia kujenga skuli 5 za ghorofa moja ikiwa na dahalia, madarasa 158, vyoo 329 na ukarabati wa skuli ya Haile Selassie.

Wakichingia taarifa hizo, wajumbe wa mkutano huo wameishauri serikali ya mkoa izingatie idadi ya watu wakati inapopanga mipango ya kimaendeleo.

Mwakilishi wa jimbo la Mfenesini, Machano Othaman Said, alisema sensa ya mwaka 2012, mkoa wa Mjini Magharibi ulikuwa na asilimia 49 ya watu wote wa Zanzibar hali ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 53 katika sensa ya mwaka huu.