OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkutano wa wadau wa sheria kuhusu utoaji wa huduma za kisheria kwa watoto wanaokinzana na sheria
HabariHabari MpyaHabari Picha

Mkutano wa wadau wa sheria kuhusu utoaji wa huduma za kisheria kwa watoto wanaokinzana na sheria

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Idrissa Kitwana Mustafa amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF kwa msaada wao mkubwa wanaoutoa katika kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wa watoto pamoja na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

Shukurani hizo amezitoa wakati akifungua mkutano wa wadau wa sheria kuhusu utoaji wa huduma za kisheria kwa watoto wanaokinzana na sheria uliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mafunzo Kilimani.

Amesema kupitia programu  ya miaka mitano iliyofadhiliwa na UNICEF, Mkoa wake umeweza kuendesha mikutano ya uhamasishaji katika ngazi ya Shehia, Skuli na Madrasa ambapo elimu juu ya uhifadhi wa mtoto na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji imetolewa kwa makundi mbali mbali wakiwemo wanawake, vijana, wanafunzi na wajasiriamali  sambamba kutoa vipindi Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Redio binafsi.

Mkuu wa Mkoa amesema pia Mkoa wake umeweza kufuatilia matukio ya udhalilishaji 2,233 ambayo yapo katika hatua mbali mbali katika vyombo vya sheria ikiwemo vituo vya polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Mahkamani.

Aidha Mkuu wa Mkoa alieleza kwamba kupitia programu hiyo Mkoa umeweza kuwaunganisha watoto waliotengana na familia zao wa ndani na nje ya Zanzibar ambapo jumla ya watoto 38 waliunganishwa na familia zao.

Mheshimiwa Idrissa ameiomba UNICEF kuendelea kutoa msaada wao katika suala zima la uhifadhi wa Watoto na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji pamoja na maeneo mengine yanayohusu wanawake na watoto na kusema kuwa  Mkoa pamoja na Wilaya zake utaendelea kufanya kazi bega kwa bega na UNICEF ili kufanikisha programu hizo.

Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amewataka wadau wa sheria kuongeza nguvu katika kielimisha jamii kufuata taratibu za kisheria katika kushughulikia masuala ya udhalilishaji badala ya kuyamaliza kifamilia.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Mtoto wa UNICEF nchini Tanzania Bibi Maud Porlyn amesema huduma za kisheria ni muhimu sana kutolewa kwa kila mtu anaehitaji hasa watoto.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano 2022-2027 shirika lake litatoa umuhimu zaidi juu ya uhifadhi kwa makundi yenye mazingira magumu dhidi ya vitendo hatarishi.

Aliwataka wadau hao wa sheria kutafuta njia bora zitakazohakikisha kila mtoto anapata huduma za kisheria na vilivile ziwe  endelevu Mjini na Vijijini.

Bi. Maud amesema UNICEF inathamini sana juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya kuhifadhiwa.

Amesema Shirika lake litaendeleza mashirikiano yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujenga mfumo wa uhifadhi wa mtoto ikiwemo kuwapatia msaada wa kisheria kwa uhuru na wakati unaohitajika.

Mada nne ziliwasilishwa katika mkutano huo ikiwemo mfumo wa hifadhi ya Mtoto Zanzibar, hali ilivyo juu ya hifadhi ya Mtoto Zanzibar, Hali halisi ilivyo kuhusu uwakilishi wa Watoto wanaokinzana na sheria Zanzibar na uzofu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar kwa wattoto wanaokinzana na sheria.