OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Watendaji Manispaa watakiwa kubadilika
HabariHabari Mpya

Watendaji Manispaa watakiwa kubadilika

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi idrissa Kitwana Mustafa amewataka watendaji na wafanyakazi wa Baraza la Manispaa Mjini   kubadilika katika utendaji wa kazi zao.

Amesema baadhi wa wafanyakazi hawatimizi wajibu wao ipasavyo na hivyo kupelekea Manispaa hiyo kushindwa kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu yake mbali mbali ya msingi.

Mkuu wa Mkoa ametoa onyo hilo katika mkutano wake na viongozi na watendaji  wa Baraza la Manispaa Mjini uliyofanyika Ofisi ya  Manispaa  hapo Malindi.

Amesema bado  kasi ya utendaji wa Manispaa hiyo hairidhishi kwa upande wa usafi wa mji, ukusanyaji wa mapato na maeneo mengine wanayoyasimamia na kutolea mfano wa shughuli za biashara ndogo ndogo na uegeshaji wa magari kuwa zimekuwa zikifanyika kiholela katika maeneo mbali mbali ya mjini.

Amewataka watendaji hao kila mmoja kujitathmini  kwa kiasi gani anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa majukumu aliyopangiwa kabla ya Serikali kuanza kuwachukulia hatua zinazostahiki.

Mkuu huyo wa Mkoa amekemea vikali pia tabia ya baadhi ya wafanyakazi kuendelea kufanya vitendo vya hujuma na ubadhirifu katika ukusanyaji wa mapato mambo ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuleta mabadiliko kwenye Manispaa hizo.

Akizungumzia suala la uwekezaji, Idrissa amewataka watendaji wa Manispaa hiyo kuwa wabunifu na kufikiria kuwekeza katika miradi  itakayoweza kuiongezea mapato Serikali  badala ya kuendelea kutegemea mapato katika vyanzo vilivyozoeleka.

Amesema licha  ya muda mrefu Serikali kuyataka Mabaraza ya Manispaa kuanzisha  miradi mikubwa, bado hakuna Manispaa yoyote kwenye Mkoa huo iliyofanya uwekezaji wa aina hiyo hadi sasa.

Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amelitaka Baraza la Manispaa Mjini kuzitumia sheria ndogo ndogo za faini za papo kwa papo kwa watu watakaohusika na kutupa taka ovyo na mambo mengine yanayokwenda kinyume na sheria zao.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini Ali Khamis Mohammed amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa maagizo aliyoyatowa watayafanyia kazi pamoja na kuzisimamia sheria zao bila ya kumuonea mwananchi yeyote.