OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Shilingi bilioni 118.6 zatumika Mkoa Mjini Magharibi.
HabariHabari Mpya

Shilingi bilioni 118.6 zatumika Mkoa Mjini Magharibi.

Kiasi cha shilingi bilioni 118.6 zitatumika kwa ujenzi wa miradi ya maendeleo itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru 2023 katika Wilaya tatu za Mkoa Mjini Magharibi.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema hayo wakati akitoa taarifa juu ya mbio za Mwenge wa Uhuru  katika Mkoa wake mbele ya vyombo vya habari hapo afisini kwake Vuga.

Amesema katika fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni 65.0 zitatumika kwa kwa miradi katika Wilaya ya Magharibi ‘A’, Wilaya ya Magharibi ‘B’ bilioni 53.2 na milioni 411.3  kwa Wilaya ya Mjini.

Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa baadhi ya miradi hiyo imo miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya maji, masoko pamoja na miradi midogo midogo ya wananchi.

Aidha Idrissa ameongeza  kwamba Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake utapita kukagua shughuli za afya ya jamii, miradi ya vijana, upandaji wa miti,  uwekaji wa mawe ya msingi sambamba na kushiriki katika kazi za ujenzi wa taifa.

Mkuu wa Mkoa amewahimiza wananchi wa Mkoa huo na Mikoa mengine ya Unguja kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru siku ya Jumatatu tarehe 29 Mei, 2023 saa 12:00 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ukitokea Mkoa wa Dar-es Salaam.

Aidha amewataka pia viongozi wa majimbo wadi na shehia kushiriki kikamilifu katika miradi yote ambayo Mwenge wa Uhuru utapita kwenye maeneo yao.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Mjini Magharibi amesema kwamba wamejipanga vizuri katika suala zima la ulinzi tangu Mwenge wa Uhuru utakapowasili katika Mkoa wake mpaka utakapokabidhiwa kwa Mkoa wa Kusini Unguja siku ya Alkhamis tarehe 1 Juni,2023 kuendelea na mbio zake.

Mwenge wa Uhuru utaanza mbio zake katika Wilaya ya Mjini siku ya Jumaatatu tarehe 29 Mei, siku ya jumanne Wilaya ya Magharibi ‘A’ na  siku ya jumatano utakimbizwa katika Wilaya ya Magharibi ‘B’.