OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mpango Mkakati tumaini kwa wasichana – Dkt. Mwinyi
HabariHabari Mpya

Mpango Mkakati tumaini kwa wasichana – Dkt. Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua Mpango Mkakati pamoja na mradi wa Tumaini wa kuzalisha taulo za wasichana kwa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF).

Uzindizi huo umefanyika kwenye maadhimisho ya mwaka moja tangu kuanzishwa kwa  Taasisi hiyo huko  katika  ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Kiembe Samaki.

Ameeleza kufurahishwa kwake na kazi nzuri inayofanywa na Taasisi hiyo na kuipongeza   kwa jithada zake za kuiunga mkono Serikali katika kuinua juhudi za kina mama na vijana wanaojishuhulisha na Kilimo cha Mwani kwa kuwapatia mafunzo pamoja na vifaa.

Aidha Dkt. Mwinyi amezungumzia suala la lishe bora kwa kinamama wajawazito na  watoto na  kusema takwimu zinaonesha  kwa wastani  watoto wawili kati ya watoto kumi wamekosa lishe bora  jambo ambalo linaweza kuepukika.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na muanzlishi wa Taasisi ya ZMBF Mama Mariam Mwinyi ameelezea mafanikio walioyapata katika kipindi cha mwaka mmoja  kuwa ni pamoja na utekelezaji wa programu mbalimbali ikiwemo Uzalishaji na ugawaji wa Taulo za  wasichana, utowaji wa Boti  pamoja   na Mafunzo ya ujengaji uwezo kwa  wakulima wa mwani.

Kadhalika amesema taasisi  hiyo imeweza kufanikiwa kutokana na michango ya kifedha, vifaa, pamoja na utaalamu wanaoupata kutoka kwa wadhamini mbali mbali katika kutekeleza programu zake na kutaja baadhi ya mashirika yakiwemo Benjameni Mkapa Foundation,  Shirika la Pact, Ubalozi mdogo wa China pamoja na Mashirika mengine.

Akizungumzia kuhusu mipango ya muda mrefu kwa taasisi hiyo Mkurugenzi wa ZMBF  Mwanaidi Ali  amesema wameandaa Mpago Mkakati wa miaka mitatu  ambao utahusisha programu mbalimbali zitakazowahusu Vijana, Kinamama pamoja na makundi mengine ambao unatarajiwa kugharimu kiasi cha shillingi millioni 2 za kimarekani katika utekelezaji wa  mkakati huo.

Nae mmoja kati ya wanufaika wa ZMBF Safia Hashim ameeleza namna taasisi hiyo ilivyobadilisha maisha yao kwa kuwapatia msaada wa vifaa  wakulima wa mwani ikiwemo boti 17. Aidha ameushukru uongozi wa ZMBF kwa namna wanavyowapatia mashirikiano kila wanapohitaji misaada ya kuendesha shughuli zao

Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora  Foundation ilianzishwa Julai 2021 na kuzinduliwa  rasmi Febuari 2022 na muanzilishi wake Mama Mariam  Mwinyi  Mke wa Rais wa Zanzibar.