OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Rc Kitwana aridhishwa na hatua za utekelezaji wa miradi ya fedha za Uviko-19 wilaya ya Mjini
HabariHabari Mpya

Rc Kitwana aridhishwa na hatua za utekelezaji wa miradi ya fedha za Uviko-19 wilaya ya Mjini

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa ameelezea kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa miradi ya maendeleo inayojengwa kupitia fedha za UVIKO 19 katika Wilaya ya Mjini. Mkuu wa Mkoa ameeleza hayo mara baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa Hospitali, Skuli na majengo ya wajasiriamali akiwa katika kukamilisha utaratibu wa ziara zake za kukagua miradi kama hiyo inayoendelea kujengwa ndani ya tatu za Mkoa Mjini Magharibi.

Amesema kwamba hatua zilizofikiwa hadi sasa katika ujenzi wa miradi hiyo inaridhisha na anaamini kwamba wakandarasi waliopewa dhamana ya ujenzi huo watamaliza ndani ya muda waliopewa. Akiwa ameambatana na baadhi ya madiwani wa wadi mbali mbali , Watendaji wa Manispaa na Wilaya ya Mjini katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi hao kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo na kuishauri Serikali pale watakapoona kuna haja ya kufanya hivyo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais wa Zanzibar kwa kuelekeza utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa katika Mkoa Mjini Mgharibi na kusema kuwa wakati itakapokamilika itaimarisha huduma za afya, elimu pamoja wajasiriamali ndani ya Mkoa wake.

Akielezea kuhusu changamoto ya malipo kwa wakandarasi wa ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Kidongo Chekundu, ameahidi kuwa uongozi Mkoa na Wilaya ya Mjini watakaa pamoja na sekta husika ili kuangalia namna ya kumaliza changamoto hiyo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amesisitiza wito wake wa kuzitaka Kampuni zilizopewa kazi za ujenzi wa miradi hiyo kuhakikisha wanawapa nafazi za kazi vijana na kinamama wa maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa hasa kwa zile kazi ambazo hazihitaji utaalamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka amesema kuwa wataendelelea kufuatilia kwa karibu ujenzi wa miradi hiyo ili kuona inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa na kumalizika kwa wakati.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Ujezi wa Hospitali ya Mkoa Mjini Magharibi na Hospitali ya Wilaya ya Mjini, Mkadiriaji Ujenzi wa Wizara ya Afya Amina Mohammed Habib amesema ujenzi wa miradi hiyo miwili unaendelea vizuri na wanatarajia kumalizika kwa muda uliopangwa.

Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alitembelea Ujenzi wa Skuli ya Msingi Kidongo Chekundu, Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa Lumumba, Hospitali ya Wilaya Chumbuni na ujenzi wa majengo ya Wajasiriamali huko Masumbani na Chumbuni.