OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>USAID yafadhili mradi wa kuwawezesha Vijana.
HabariHabari Mpya

USAID yafadhili mradi wa kuwawezesha Vijana.

Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi imeeleza kuwa itatoa  mashirikiano ya kutosha ili kufanikisha mradi  wa  miaka minne wa kuwawezesha vijana kujitegemea unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani USAID.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla alipokuwa akifungua kikao cha kutoa elimu kwa maofisa wa afya, ustawi wa jamii, vijana na mipango juu ya namna mradi huo utakavyotekelezwa katika Mkoa huo.

Akizungumza na maofisa hao pamoja na wasimamizi wa mradi huo, Katibu Tawala  amesema  Mkoa wake umefarijika sana kuja kwa mradi huo kwa vile una malengo mazuri ya kuwaendeleza vijana kielimu, kiujuzi  pamoja na  kuwapa stadi za maisha ambazo  zitawawezesha kujitegemea na kuwa na maisha bora hapo baadae.

Aidha ameeleza kuwa mradi huo unakwenda sambamba na mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwainua vijana katika nyanja mbali mbali, hivyo Mkoa pamoja na Wilaya zake zitahakikisha malengo ya mradi huo yanatimia.

Akiwasilisha maelezo juu ya utekelezaji wa mradi huo unaofahamika kama USAID – Kijana Nahodha, Meneja wa Mradi  Upendo Laizer amesema mradi huo utahusisha vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 24 wakiwemo waliyoacha Skuli,waliokuwa hawajaajiriwa na wale waliopata ujauzito katika umri mdogo ili kuwapa mafunzo mbali mbali yatakayoweza kuwaandaa waweze kujitegemea.

Amewataka maofisa wa Mkoa na Wilaya  watakaohusika na mradi huo kushirikiana katika kuwatambua vijana watakaopatiwa mafunzo hayo pamoja na maeneo na makundi watakayotoka.

Amesema kuwa kiasi cha dola za Marekani milioni 10.6 zitatukumika kwa mradi huo wa miaka minne kuanzia 2023 hadi 2026 kwa Mikoa mitano ya Zanzibar na Mikoa miwili kwa Tanzania Bara utakaosimamiwa na T-MARC Tanzania.

Kwa upande wao maofisa walioshiriki kikao hicho wametoa michango mbali mbali itakayopelekea kufanikisha mradi huo pamoja na kuahidi kutoa mashirikiano yao pale mradi utakapoanza kutekelezwa.