OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wawekezaji wametakiwa kuwekeza katika maeneo yanahusiana na Uchumi wa Buluu.
HabariHabari MpyaHabari Picha

Wawekezaji wametakiwa kuwekeza katika maeneo yanahusiana na Uchumi wa Buluu.

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umewaomba wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza katika Mkoa huo kwenye maeneo mbali mbali yanayohusina na Uchumi wa Buluu.

Umesema kwamba kupitia Uchumi wa Buluu wanaweza kuwekeza katika maeneo mbali mbali ndani ya Mkoa huo ikiwemo uvuvi, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki na bidhaa zitokanazo na mwani, ujenzi wa hoteli za kitalii pamoja na fursa nyenginezo.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa wakati akifungua mkutano wa wadau wa uwekezaji ulioandaliwa na Taasisi ya GiZ ya Ujerumani ,uliofanyika Hoteli ya Serena Inn iliopo  Shangani.

RC Kitwana akifungua Mkutano wa wadau wa Maendeleo na Taasisi ya GiZ kutoka Ujerumani

Amesema kwamba Serikali ya Awamu ya Nane inavyoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imetoa kipaumbele kikubwa katika uwekezaji kupitia Uchumi wa Buluu ili kukuza uchumi wa nchi pamoja na ajira, hivyo inawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta hiyo.

“Nawaomba wawekezaji kuja kuwekeza katika eneo hili ili kuiunga mkono Serikali kuweza kutimiza dhana ya Uchumi wa Buluu. Nataka niwahakikishie kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa mashirikiano ya dhati kwa wawekezaji watakaoonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta hii”, alieleza Idrissa.

Mbali na uwekezaji katika Uchumi wa Buluu, Mkuu wa Mkoa vilevile ametoa wito kwa wawekezaji  kuwekeza  katika maeneo yanayogusa moja kwa moja jamii ndani ya Mkoa huo  ikiwemo ujenzi wa majengo ya makaazi na biashara, masoko, maegesho ya magari na huduma nyengine.

Akizungumzia suala ya amani, Mkuu wa Mkoa  amewaeleza wadau hao wa uwekezaji kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kuilinda amani na utulivu uliopo ndani ya Mkoa huo ili kuwavutia wawekezaji zaidi kuja kuwekeza katika Mkoa wake sambamba na wale waliokwisha kuwekeza kuwa na uhakika wa uwekezaji wao.

Mkutano wa Wadau wa Maendeleo -Serena

Amesema suala la amani ni moja ya ajenda kuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na vilevile Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo watahakikisha wanailinda kwa maslahi  mapana ya Taifa.

Mkuu wa Mkoa ameipongeza Taasisi hiyo ya GiZ kwa uamuzi wao wa kufanya Mkutano huo uliowakutanisha wadau wa uwekezaji na taasisi zisizo za kiserikali na kujadiliana juu ya mambo mbali mbali yanayohusiana na suala zima la uwekezaji. Aliongeza  kwamba kupitia mkutano huo kutaweza kuitangaza zaidi Zanzibar Kimataifa.

“Ni jambo la busara kuona GiZ wameamua kuja Zanzibar na kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa uwekezaji kuangalia fursa zilizopo za uwekezaji hapa Zanzibar”, alisema Idrissa.

Hivyo ameishauri Taasisi hiyo  kuangalia maeneo watakayoweza kuwashawishi wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza ndani ya Mkoa wake na Zanzibar kwa Ujumla.

Kwa upande wake Afisa wa GiZ  Richard Shaba amesema dhamira ya ujio wao ni kuja kuangalia fursa ziliopo za uwekezaji ili kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza hapa Zanzibar.

Amesema kwamba wameamua kuchukua hatua hiyo kwa makusudi kutokana na kuridhishwa kwao na utendaji wa Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi tangu ashike madaraka mwezi Novemba 2020.