OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Maoni yanayokusanywa kuhusu kanuni za kuendesha vikao vya Kamati za Maendeleo ya Mikoa yataimarisha utekelezaji- RC Kitwana
HabariHabari Mpya

Maoni yanayokusanywa kuhusu kanuni za kuendesha vikao vya Kamati za Maendeleo ya Mikoa yataimarisha utekelezaji- RC Kitwana

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema kuwa maoni yanayokusanywa kuhusu rasimu ya muongozo wa majukumu na uendeshaji wa vikao vya Kamati za Maendeleo za Mikoa yatasaidia kuboresha rasimu hiyo ili kufikia lengo lililokusudiwa.


Akifungua kikao cha kupokea maoni kuhusu rasimu hiyo katika ukumbi wa mikutano ofisini kwake Vuga, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa anaamini mawazo yatakayotolewa na wajumbe wa kikao hicho yatafanyiwa kazi ili kuona Kamati za Maendeleo za Mikoa zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Amesema Mkoa wake umefarajika na mpango huo unaotekelezwa na Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwavile utavipa nguvu vikao vya Kamati za Mendeleo za Mikoa katika kuamua na kusimamia miradi itakayotekelezwa ndani Mikoa yao.


Akizungumzia kuhusu zoezi hilo la kukusanya maoni mwanasheria kutoka Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Fidelis Mauru amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kupata maoni yatakayopelekea kuimarisha muongozo wa majukumu ya uendeshaji wa vikao vya Kamati za Maendeleo za Mikoa.


Amesema Wizara yake imebaini uwepo wa utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ndani ya Mikoa bila ya mahitaji halisi, hivyo hatua hiyo itasaidia kuondosha changamoto hiyo kupitia Kamati za Maendeleo za Mikoa.
Nao watendaji wa sekta mbali mbali kutoka Mkoa, Wilaya na Manispaa za Mkoa Mjini Magharibi pamoja na taasisi nyengine za Serikali walioshiriki kikao hicho waliotoa maoni yao ili kuboresha rasimu hiyo.