OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Rais Mwinyi kuzindua Darajani Souk
HabariHabari Mpya

Rais Mwinyi kuzindua Darajani Souk

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuzindua rasmi kituo cha biashara cha Darajani Souk siku ya Jumaamosi ya tarehe 18/02/2023.

Taarifa rasmi juu ya uzinduzi wa kituo hicho imetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akizungumza na  vyombo vya habari kuhusiana na uzinduzi wa mradi huo hapo Darajani.

Amesema ujenzi wa kituo hicho cha kisasa chenye maduka 452, bustani na eneo la kuegesha magari tayari umeshakamilika na matayarisho mbali mbali ya uzinduzi wake yanaendelea vizuri.

Mkuu wa Mkoa amewaomba wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi na Mikoa mengine jirani kuhudhuria kwa wingi kwenye uzinduzi wa mradi huo ambao amesema mbali na kubadilisha mandhari ya eneo la Darajani vile vile utatoa fursa nyingi zaidi kwa wafanyabiashara  kuendesha shughuli zao.

Amesema kwamba tayari mpango mzuri wa kuendesha biashara  umeshapangwa ili kurahisisha  upatikanaji wa bidhaa mbali mbali  zitakazouzwa katika kituo hicho yakiwemo mavazi, vifaa vya kiektroniki na huduma nyenginezo.

Mhe. Idrissa amewahakikishia wafanyabishara waliokuwepo kabla ya ujenzi huo kuwa watarudi kuendesha  biashara zao mahala hapo na nafasi zitakazobaki watapewa wafanyabiashara wengine waliyoomba kukodi milango ya biashara kwenye eneo hilo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maelekezo yake yaliyopelekea kufanikisha ujenzi wa mradi huo katika eneo hilo la Darajani.

Ujenzi wa  Darajani Souk uliogharimu  kiasi ya shilingi bilioni nane ulianza mwezi februari mwaka 2022 huku awamu ya pili ya  mradi huo ikitarajiwa kuanza hivi karibuni na kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023.