OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>ZECO yaimarisha nishati ya umeme kupitia mradi wa ZESTA
HabariHabari Mpya

ZECO yaimarisha nishati ya umeme kupitia mradi wa ZESTA

Mkuu wa Wilaya Magharibi “A” Mhe. Suzan P. Kunambi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi ameendesha kikao baina ya ZECO na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, kuhusu mradi wa kuimarisha sekta ya Nishati na upatikanaji wa huduma ya umeme Zanzibar (ZESTA).

Mhe. Suzan amewaahidi kuwapa mashirikiano yote ili mradi huo wa umeme ufanikiwe na kuleta tija kwa jamii.

Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Nd. Moh’d Ali Abdalla alisisitiza kufuatwa taratibu za manunuzi kwa kunuliwa vifaa bora vitakavyotumika katika mradi ili kuufanya mradi huo kuwa endelevu na kuleta tija kwa Serikali na Wananchi kiujumla.

Meneja Mradi wa ZESTA amesema mradi huu utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 142 Mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo utatekeleza kwa kipindi cha miaka 6, na ZECO wamejipanga kuufanya mradi huu kuwa endelevu kwa kuwajengea uwezo wahandisi wa Shirika kuweza kuuendeleza mradi huu ili kuboresha nishati za umeme visiwani Zanzibar.

Msaidizi Meneja wa Mradi wa ZESTA amesema katika Mkoa wa Mjini Magharibi mradi utapita Wilaya ya Magharibi “A” katika Shehia mbalimbali ikiwemo Welezo, Hawaii, Mchikichini na Mwera ambapo katika eneno la Welezo kutajengwa kituo cha kupokea umeme pamoja na betri za kuhifadhia umeme zenye uwezo wa kuhifadhi umeme wa megawati 20.

Akiwasilisha Mada katika kikao hicho Afisa ustawi wa jamii kutoka ZECO alieleza katika utekelezaji mradi huo kutakuwa na mfumo wa kutatua changamoto za wananchi zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi ikiwemo fidia ya majengo, ardhi, vipando, vitendo vya udhalilishaji, mgawanyo wa ajira kwa wazawa na yatakayojitokeza wakati wa utekelezaji, ambapo kamati mbambali zimeundwa kuanzia ngazi ya Shehia, Wilaya, ZECO, Mkoa, Wizara na Mahakama kwa migogoro itakayokosa utatuzi kwa ngazi za chini.

Nae Afisa Kazi Mkoa Mjini Magharibi amesisitiza kufuatwa taratibu na miongozo ya ajira kwa kukatwa vibali vya kazi pamoja kuweka utaratibu mzuri wa kutoa kipaumbele kwa wazawa wa maeneo ambayo mradi huo utapita.

Aidha washiriki wa kikao wameishukuru ZECO kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi za Mhe. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi kwa kuwaletea wananchi nishati ya Umeme wa Uhakika katika maeneo yote.

Vile vile wameishauri ZECO kuendelea kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya utekelezaji wa mradi huo ili kuweza kufikia malengo ya Serikali kwa ujumla.