OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mjini Magharibi Waomba Kupewa Kipaumbele
HabariHabari Mpya

Mjini Magharibi Waomba Kupewa Kipaumbele

Imeelezwa kuwa kutokana na matokeo ya sensa ya watu na  makaazi ya mwaka 2022 kuna haja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuupa kipaumbele Mkoa Mjini Magharibi katika mipango yake mbali mbali ya maendeleo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa katika kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa  shughuli za Mkoa huo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba  2022 mbele ya Kamati ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakililishi  kilichofanyika ukumbi wa KVZ Mtoni.

Amesema kwa mujibu wa sensa hiyo asilimia 47.3 ya watu wote wa Zanzibar wanaishi katika Mkoa Mjini Magharibi hali inayoonesha kuwa mahitaji ya huduma mbali mbali za kijamii ni makubwa zaidi  kwenye mkoa huo ikilinganishwa na mikoa mingine ya Zanzibar.

Amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kulishawishi Baraza la Wawakilishi na Serikali  kuongeza kasma ya miradi mbali mbali ya maendeleo kwa Mkoa Mjini Magharibi ili iweze kukidhi mahitaji ya wakaazi wake.

Akijibu hoja ya wajumbe wa kamati hiyo  kuhusu vikundi vya vijana vinavyofanya uhalifu kwenye shehia mbali mbali za Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa amesema  Kamati ya Usalama ya Mkoa imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na vikundi hivyo na tayari wameanza kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria vijana wanaofanya vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Machamo Othman Said ameitaka Serikali ya Mkoa huo kuchukua juhudi zaidi kukabiliana na vitendo vya uhalifu na kusema kuwa kama Mkoa utajipanga vizuri zaidi upo uwezekano ndani ya muda mfupi vitendo hivyo vikadhibitiwa.

Aidha ameushauri  Mkoa kuongeza vituo vidogo vya polisi katika mitaa na kutumia askari wa vikosi vya SMZ kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuimarisha amani na utulivu kwenye Mkoa huo.

Nao wajumbe wa Kamati hiyo wameutaka Mkoa kuchukua juhudi za ziada katika kukabiliana na tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya udhalilishaji kwa vile  takwimu zinaonesha bado vitendo hivyo viko juu ndani ya Mkoa huo.

Awali kamati hiyo ilipokea taarifa ya shughuli mbali mbali zilizotekelezwa na Mkoa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022-2023 likiwemo suala la ulinzi, anuani ya makaazi, mikopo nafuu ya wajasiriamali,  watu wenye ulemavu, utatuzi wa migogoro ya ardhi, kero za wananchi pamoja na kuratibu shughuli za sekta mbali mbali za Serikali.