OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Rc Kitwana awaapisha Masheha wapya
HabariHabari Mpya

Rc Kitwana awaapisha Masheha wapya

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa kitwana Mustafa amewaapisha Masheha wapya wa baadhi ya Shehia katika Wilaya ya Magharibi A na Wilaya ya Magharibi B aliyowateua hivi karibuni.

Waliyoapishwa kwa Wilaya ya Magharibi A ni  Rehema Ame Khatib wa Shehia ya Mtofaani, Khamis Ussi Juma wa Shehia ya Kijichi, Khatib Haroub Khatib wa Shehia ya Kikaangoni na Zahra Hassan Mohamed wa Shehia ya Mtoni. Kwa upande wa Wilaya ya Magharibi B ni Omar Bakari Simba wa Shehia ya Uzi.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Masheha hao katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Mhe. Idrissa amewataka Masheha wa Mkoa huo kusimamia ipasavyo utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Shehia zao.

Amesema kama viongozi wa Serikali katika ngazi ya Shehia wana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 kwa vile ndio ilani inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Mkuu wa Mkoa  amewataka pia masheha kuwa wepesi katika kuwatumikia wananchi pale wanapohitaji huduma mbali mbali ziliyomo kwenye mamlaka yao pamoja na kuwapa maelekezo mazuri pindi wakihitaji huduma hizo katika ngazi ya juu ya Serikali.

Aidha Mhe. Idrissa amewaasa Masheha kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao  na kuwataka wajiepushe na vitendo ambavyo vineweza kusababisha migogoro katika utendaji wa kazi zao.