OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa Mjini Magharibi Wamiminiwa Pongezi.
HabariHabari Mpya

Mkoa Mjini Magharibi Wamiminiwa Pongezi.

Mkoa Mjini Magharibi umepongezwa kwa kuonesha uzalendo na mashirikiano makubwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2023 ndani ya Mkoa huo.

Pongezi hizo zimetolewa na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wakiongozwa na  Kiongozi wao Abdallah Shaibu Kaimu walipokuwa wakiaga kuelekea Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika Tunguu.

Wamesema kwamba kitendo cha viongozi wa Mkoa, Wilaya, taasisi za Serikali, vyama vya siasa pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizo kimewapa faraja sana na kutaka mikoa mengine ya Zanzibar na Tanzania Bara kuiga mfano huo.

Wamepongeza pia namna vijana  walivyohamasika na kushiriki kwa wingi  katika Wilaya zote tatu za Mkoa Mjini Magharibi na kushauri vijana hao waendelee kutumika katika matukio mbali mbali  ya kijamii na kitaifa ili kuwajengea uzalendo wa kutumikia nchi yao.

Aidha wameusifu Mkoa Mjini Magharibi kwa kukimbiza Mwenge wa Uhuru masafa marefu kwa miguu ndani ya Wilaya zake tofauti na Mikoa mengine yote waliyokwisha pita tangu mbio za Mwenge wa Uhuru zilipozinduliwa Mkoani Mtwara tarehe 1 Aprili,2023.

Kwa upande mwigine wamepongeza Mkoa na Wilaya zake kwa kutekeleza kwa vitendo maeneo tofauti ya ujumbe wa Mwenge wa uhuru likiwemo suala la utunzaji wa mazingira, mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, malaria na lishe bora.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Abdallah Shaibu Kaimu aliwataka viongozi wa Mkoa huo kuongeza juhudi za kuwatumikia wananchi ili kufikia malengo ya Serikali zote mbili ya kuwaletea maendeleo wananchi. Katika makabidhiano hayo  Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa aliukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid kuanza mbio zake katika Mkoa huo.