OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>“Jukumu la kuwapatia elimu vijana sio la Serikali pekee bali ni la watu wote” RAS
HabariHabari Mpya

“Jukumu la kuwapatia elimu vijana sio la Serikali pekee bali ni la watu wote” RAS

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umesema kwamba utahakikisha unaimarisha mashirikiano baina ya wazazi, walimu na wanafunzi ili kuinua kiwango cha elimu na ufaulu katika Mkoa huo.

Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla amesema hayo mara baada ya kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa darasa la nne, saba, kidatu cha pili na nne kwa mwaka 2022 kwa Mkoa huo.

Amesema jukumu la kuwapatia elimu vijana sio la Serikali pekee bali ni la watu wote, hivyo kikao hicho kimetoka na maazimio mbali mbali moja wapo ni kuona kamati za wazee za Skuli, Masheha, wazazi na walezi wanashiriki kikamilifu katika suala la elimu ya watoto wao.

Aidha amesema katika kikao hicho cha tathmini kimeweka pia malengo ya muda mfupi na muda mrefu ambayo yanakwenda sambamba na mipango ya Serikali ya kuinua kiwango cha elimu nchini.

Afisa Elimu Mkoa Mjini Magharibi Mohammed Abdallah Mohammed amesema licha ya ufaulu wa wanafunzi wa kidatu cha pili, nne na sita kuongezeka kila mwaka katika Mkoa huo bado kuna haja ya kuongeza mikakati ili kupata matokeo mazuri zaidi.

Naye Afisa taaluma Wilaya ya Magharibi B Ahmed Abdulmajid Shaaban amesema kuwa iwapo wazazi watashiriki kikamilifu pamoja na kudhibiti tatizo la utoro wa wanafunzi upo uwezekano mkubwa wa kuongeza kiwango cha ufaulu.

Kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Tawala Mkoa kilishirikisha maofisa elimu na maofisa taaluma kutoka Mkoa, Wilaya ya Mjini, Wilaya ya Magharibi A na Magharibi B.