OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Taarifa ya kufanya mabadiliko ya kuimarisha elimu ya msingi kwa kurejesha darasa la saba, Zanzibar
HabariHabari Mpya

Taarifa ya kufanya mabadiliko ya kuimarisha elimu ya msingi kwa kurejesha darasa la saba, Zanzibar

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(Ijumaa 24/12/2021)

Ndugu waandishi wa habari,

Sera ya Elimu ya mwaka 2006 inaelekeza elimu ya Msingi ya Miaka Sita kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la sita. Kufuatia Sera hiyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ilifanya mabadiliko ya mfumo wa elimu wa Zanzibar ambapo pamoja na mambo mengine Wizara iliondosha elimu ya darasa la saba kwa kuweka ukomo wa elimu ya msingi hadi darasa la sita. Lengo la Wizara lilikuwa ni kumuwezesha mwanafunzi kuweza kupata fursa za elimu ya maandalizi, msingi na sekondari akiwa na umri muafaka utakaomuwezesha kupata fursa za kujiunga na elimu ya juu mapema kama nchi nyingi zilivyo. Sera hiyo pia ilielekeza elimu ya maandalizi iwe ni sehemu ya elimu ya lazima kwa muda wa miaka miwili.

Ndugu waandishi wa habari,

Baada ya kuanzishwa kwa dasara la sita wadau mbalimbali waliweza kutoa maoni yao juu ya uwezo wa wanafunzi kwa kulinganisha umri, idadi ya masomo na uwezo wa kukabiliana na masomo hayo wakiwa katika ngazi ya msingi na maendeleo yao watakapoingia elimu ya sekondari. Aidha, kutokana na mabadiliko mbalimbali na mikakati ya maendeleo nchini pamoja na changamoto tofauti zinazoikabili sekta ya elimu, Wizara imeona ipo haja ya kufanya tathmini kwa kina na kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Ndugu waandishi wa habari,

Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imepanga kufanya mabadiliko katika ngazi ya elimu ya msingi kwa kurejesha darasa la saba. Mabadiliko haya yataifanya elimu ya msingi kuwa ni ya miaka saba badala ya sita kama ilivyo sasa kuanzia mwaka 2022. Ikumbukwe kua uamuzi huu unafuatia maoni na ushauri uliotolewa katika mijadala mbalimbali ya wadau wa elimu. Wadau walitoa hoja ya kuwa watoto wanaoanza elimu ya sekondari kidato cha kwanza bado ni wadogo na hawajajitambua vizuri hali ambayo inawapa ugumu kuyakabili masomo yao ya ngazi ya sekondari kiasi ambacho kinawapelekea kufanya vibaya katika mitihani yao ya taifa ya sekondari. Wizara imeyajadili kwa kina maoni hayo yote ambayo utekelezaji wake utafuata awamu kwa awamu kwa kuzingatia muda muafaka. Wizara imeyakubali na kuamini kuwa kurejesha darasa la saba ni mabadiliko yanayopaswa kufanywa kwa harasa kwani inaamini yatasaidia sana kumtayarisha mwanafunzi vizuri katika maendeleo yake ya elimu na pia yatachangia sana katika maandalizi ya mwanafunzi kuweza kuyamudu vyema masomo yake ya elimu ya sekondari kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na kijamii kwa sasa.

Ndugu wandishi wa habari,

Mfumo wa elimu wa darasa la saba utatekelezwa rasmi kuanzia mwaka wa masomo 2022 ambapo mahitaji yote ya msingi yakiwemo mitaala, walimu, vitabu na madarasa vimezingatiwa na kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuanza darasa hilo.

Ndugu wandishi wa habari,

Kwa upande wa Mtaala, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mabadiliko ya mtaala wa ngazi ya maandalizi na msingi. Mtaala umezingatia mabadiliko mbalimbali yakiwemo kupunguza idadi ya masomo ambayo yalioneka ni mengi ukizingatia na hali halisi ya watoto wetu katika kujifunza. Aidha, kwa upande wa darasa la saba mitaala imezingatia mabadiliko hayo.

Ndugu wandishi wa habari,

Kwa upande wa Walimu, Wizara imefanya tathmini na kuona kuwa walimu waliopo katika ngazi ya maandalizi na msingi wanatosheleza kufundisha katika ngazi hiyo likiwemo darasa la saba. Wizara haina mashaka na uwezo wa walimu hao katika kufundisha darasa la saba kwani walimu hao tayari wamethibitiswa kufundisha ngazi ya elimu ya maandalizi na msingi kwa kila somo.
Aidha, baada ya kukamilika kwa mtaala, Wizara imejipanga kuwapatia Mafunzo walimu wote wa msingi ili kuendana na matakwa ya mtaala mpya.

Ndugu wandishi wa habari,

Kwa upande wa vifaa vya kufundishia na kujifunza, Wizara itatayarisha vifaa vyote vikiwemo vitabu vitakayo tumika katika ufundishaji wa elimu ya msingi likiwemo darasa la saba. Aidha, vitabu vilivyopo sasa pia vinaweza kutumika kwa kuanzia wakati Wizara inatayarisha vitabu vipya, hii inatokana na kuwa hakutokuwa na mabadiliko makubwa ya mada zinazopaswa kusomesha elimu ya msingi, ila mabadiliko yanaweza kutokezea kwa mada na darasa husika.

Ndugu wandishi wa habari,

Ni dhahiri kwamba kuongezeka kwa darasa la saba kutapelekea ongezeko la mahitaji ya madarasa kwa wanafunzi wa ngazi ya maandalizi na msingi. Kwa upande mwingine ngazi ya elimu ya sekondari itakuwa na upungu wa wanafunzi kwani siwote wanaomaliza darasa la sita wataendelea elimu ya sekondari ya kidato cha kwanza kama ilivyo sasa. Kufuatia mazingira hayo Wizara itarekebisha hali ya miundombinu kwa mujibu wa mahitaji halisi ya kila upande.

Ndugu wandishi wa habari,

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inatarajia mabadiliko haya yataleta mafanikio makubwa katika elimu ya msingi kwani wanafunzi watapata matayarisho makubwa katika kujifunza masomo ya elimu ya msingi na kuwawezesha kuwa na uwezo mzuri wa kuanza masomo ya sekondari na hivyo kutoa wanafunzi wengi katika ufanisi bora.

Ndugu wandishi wa habari,

Baada ya maelezo hayo mafupi, niwashukuruni sana kwa ushirikiano wenu na ahsanteni sana kwa kunisikiliza.