OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>“Dira ya Maendeleo 2025-2050 ikidhi mahitaji ya Taifa”- RC Kitwana
HabariHabari Mpya

“Dira ya Maendeleo 2025-2050 ikidhi mahitaji ya Taifa”- RC Kitwana

Imeelezwa kuwa ushirikishwaji mpana wa wadau mbali mbali katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050 utawezesha kupata Dira jumuishi yenye kukidhi mahitaji stahiki ya Taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Hayo yameeleza na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akifungua semina ya uelimishaji umma kuhusu Maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050 kwa viongozi na makundi mbali mbali ya Mkoa Mjini Magharibi.

Amesema warsha hiyo kwa viongozi wa Mkoa, Wilaya, Mabaraza ya Manispaa pamoja na makundi mbali mbali imeweza kuwajengea uelewa mpana pamoja na kufahamu majukumu yao yatakayosaidia kufanikisha shughuli hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Mkuu wa Mkoa amesema semina za aina hiyo ni muhimu kwavile  zitatoa fursa kwa wadau  kuweza kutoa maoni na kujadili kwa kina kuhusu mipango ya Taifa kwa miaka 25 ijayo, hivyo  amewataka viongozi hao na makundi mbali mbali kuitumia kikamilifu fursa hiyo kwa kutoa maoni yao.

Aidha Idrissa ameishauri timu ya uandishi wa Dira 2025-2050 kuzingatia michango na maoni yatakayotolewa ili kuweza kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amepongeza utaratibu wa kutoa elimu kupitia vipeperushi, mabango na vyombo vya habari na kusema kuwa utasaidia kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu maandalizi ya Dira hiyo.

Akiwasilisha mada kuhusu Maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025-2050, mjumbe kutoka Kamati ya Maandalizi Moza Ramadhani Omar amesema kuwa utaratibu wa kukusanya maoni unaendelea katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, lengo ni kupata maoni yatakayosaidia kuiboresha Dira hiyo.

Ameuomba uongozi wa Mkoa kuchukua kila juhudi kuwahamasidha wananchi wa Mkoa huo kuweza kujitokeza kutoa maoni yao wakati zoezi la uelimishaji na ukusanyaji maoni likifanyika katika ngazi ya Wilaya na Shehia.

Amesisitiza kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kutategemea sana namna Mkoa na Wilaya zake watakavyohamasisha na kuratibu vizuri ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi na  makundi mbali mbali.

Wakitoa michango yao katika warsha hiyo wajumbe wameshauri suala la elimu na maadili litiliwe mkazo katika Dira hiyo ili kuwa na kizazi bora cha taifa la baadae.

Vilevile wametaka kuwekwa mikakati imara ya kuwawezesha vijana na kukuza uchumi, ili kuenda sambamba na kasi ya maendeleo ya Dunia.

Warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Afisi ya Mkuu wa Mkoa ilihudhuriwa na Viongozi wa Mkoa, Wilaya, Mabaraza ya Manispaa, taasisi za dini na makundi mbali mbali.