OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC atoa wito wananchi kushiriki Maadhimisho ya Muungano
HabariHabari Mpya

RC atoa wito wananchi kushiriki Maadhimisho ya Muungano

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye matukio mbali mbali  yatakayofanyika ndani ya Mkoa huo katika Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza na vyombo mbali mbali vya habari hapo Afisi ya Mkuu wa Mkoa Vuga kuhusiana na maadhimisho hayo, ameyataja matukio yatakayofanyika ni pamoja na usafi wa mazingira, uzinduzi wa Skuli ya Msingi Kidongo Chekundu, Kongamano na Sherehe za Kilele cha Maadhimisho hayo.

Amefahamisha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Skuli  tarehe 24 April na Kongamano Tareha 25 April katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip.

Kwa upande wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano,Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa wanatarajia wanasiasa mashuhuri  kuja kuwasilisha mada ikiwemo Umuhimu wa Muungano katika Bara la Afrika, Historia na Umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Fursa zilizopo kwa Vijana ndani ya Muungano.

Aidha Idrissa ameeleza kuwa  Maadhimisho ya Muungano kwa mwaka huu yanafanyika katika ngazi ya Mikoa kote nchini, hivyo kwa Mkoa wake kilele cha Maadhimisho hayo kitafanyika katika viwanja vya Maisara, Wilaya ya Mjini ambapo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa husika.

Amesema katika kilele hicho wafanyakazi wa taasisi za Serikali, binafsi, wanafunzi wa Skuli za Sekondari na elimu ya juu, jumuia, viongozi, wanachama na wapenzi wa vyama vya siasa, makundi maalum pamoja na wananchi  ni muhimu kuhudhuria ili kuonesha namna wanavyothamini jitihada zilizochukuliwa na Waasisi wa Muungano Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere.

Mkuu wa Mkoa ameeleza pia ushiriki mkubwa wa wananchi mkubwa kwenye kilele hicho kutadhihirisha namna wanavyounga mkoa juhudi zinazochukuliwa na viongozi wakuu wa nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuulinda Muungano na kuwaletea maendeleo wananchi.

Kwa upande Mwengine Idrissa ameviomba vombo vya habari kushiriki kikamilifu kwenye matukio yote ili kuweza kuwahabarisha wananchi yale yote yatakayofanyika katika Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano kwenye Mkoa Mjini Magharibi.