OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mradi wa USAID-Kijana Nahodha wazinduliwa.
HabariHabari Mpya

Mradi wa USAID-Kijana Nahodha wazinduliwa.

Vijana nchini wametakiwa kuzichangamkia fursa zitakazopatikana kupitia mradi wa Shirika la Misaada la Marekani USAID unaojulikana kama Kijana Nahodha ili waweze kutimiza ndoto zao.

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika hotuba yake wakati akizindua mradi huo hapo viwanja vya Maisara, Wilaya ya Mjini.

Amesema kwamba katika mradi huo vijana wapatao 15,000 wa Zanzibar wataweza kupatiwa  elimu juu ya masuala ya utalii, kilimo, ufugaji, ujasiriamali pamoja na stadi za maisha hatua ambayo itawawezesha kujitegemea kimaisha.

Dk. Mwinyi amezitaka sekta zote za Serikali zinazohusika na mradi huo kushiriki ipasavyo pamoja na kufuatilia utekelezaji wake ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.

Kwa upande mwengine Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya awamu ya nane inaendelea na jitihada zake za kuwawezesha vijana kwa ujenzi wa majengo ya wajasiriamali kila Wilaya, ujenzi wa vyuo vya amali kila Mkoa na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu.

Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Kijana Nahodha Bi. Tuhuma Tuli  amesema  mradi huo umelenga kuwapatia  mafunzo ya fani mbali mbali pamoja na elimu afya ya mwili na akili vijana  kuanzia umri wa miaka 15 hadi 25 wakiwemo waliyoacha skuli, waliopata ujauzito katika umri mdogo, walemavu na wasio na ajira.

Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Misaada la Marekani USAID Kate Somvongsiri  ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake inazochukuwa za kuwawezesha vijana na kusifu mashirikiano wanayoyapata katika kutekeleza mradi wa Kijana Nahodha.

Jumla ya Vijana 45,000 kutoka mikoa miwili ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar watanufaika na mradi huo wa miaka minne uliyoanza Septemba 2022 hadi Ogasti 2026.