OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa Mjini Magharibi wapongezwa kwa kufanikisha zoezi la Sensa 2022
HabariHabari Mpya

Mkoa Mjini Magharibi wapongezwa kwa kufanikisha zoezi la Sensa 2022

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makaazi Balozi Mohammed Hamza ameupongeza uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi kutokana na mashirikiano yao makubwa yaliyopelekea kufanikisha zoezi la sensa katika Mkoa huo.

Amesema Mkoa Mjini Magharibi umefanya vizuri katika zoezi hilo kutokana na  kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa  Mkoa, Wilaya na Shehia ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa hiyo.

Balozi Hamza amesema hayo wakati  alipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi kutoa shukurani zake kwa Uongozi wa Mkoa huo kwa  kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi lilofanyika mwezi Ogasti mwaka huu.

Amesema wasimamizi wa sensa na makarani wao walifanya kazi nzuri ambapo taarifa zote zilizohitajika ziliweza kukusanywa kwa zaidi ya asilimia 99 ya majengo na watu wakiwa wamehesabiwa kwenye Mkoa huo.

Akizungumzia matokeo ya sensa ya mwaka 2022, Balozi Hamza amesema Serikali itatoa muongozo kwa kila ngazi na kuwataka viongozi wa Mkoa, Wilaya, Shehia na wadau wengine kufuata mwongozo huo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi Idrissa Kitwana Mustafa amesema matokeo ya sensa hiyo yatakuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya Mkoa wake.

Aidha ameahidi kuwa Mkoa wake utaendeleza mashirikiano  na Ofisi ya Mtakwimu Zanzibar katika  masuala mbali mbali yatakayojitokeza kuhusu matumizi ya sensa hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis amezishukuru Serikali zote mbili kutokana na mwongozo  na maelekezo yao yaliyopelekea kufanikisha zoezi hilo.