OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa Mjini Magharibi Watangaza Operesheni Maalum dhidi ya Wahalifu
HabariHabari Mpya

Mkoa Mjini Magharibi Watangaza Operesheni Maalum dhidi ya Wahalifu

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Mjini Magharibi  imeanzisha operesheni maalum katika Shehia zote 121 za Mkoa huo ya kuwakamata watu wanaofanya vitendo vya uporaji, wizi na uhalifu.

Akitoa taarifa kuhusu operesheni hiyo, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema operesheni hiyo itafanywa na vikosi vyote vya ulinzi ili kuwatia mikononi wale wote wanaojihusisha na matendo hayo pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria.

Mkuu wa Mkoa amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ina dhima ya kusimamia suala zima la ulinzi ndani ya Mkoa huo hivyo ameonya kuwa haitachelea kumchukuli hatua mtu yoyote yule atakaebainika kujihusisha na uporaji, wizi na uhalifu wakati  operesheni hiyo ikiendelea.

Ametanabahisha kuwa Serikali ina vyanzo vya kutosha kuweza kupata taarifa za vijana wanaofanya vitendo hivyo na kuwataka wazazi na walezi kuwaelimisha  vijana wao kutojiingiza kwenye vitendo hivyo badala ya kuwalinda.

Aidha Idrissa amewataka pia Masheha na jamii  kutoa mashirikiano yao  katika operesheni hiyo kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya matendo hayo na kusema kuwa vyombo vya ulinzi itawahifadhi wale wote watakaotoa taarifa hizo.

Kwa upande mwengine  Mkuu wa Mkoa amewaasa vijana kutojiingiza kwenye vitendo vya aina hiyo kwani havina tija hata kidogo  kwao, familia zao na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kusimamia  suala zima la amani  na utulivu ndani ya Mkoa huo ili waweze  kuendelee na shughuli zao za maisha kama kawaida.