OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Ziara ya Mhe. Hemed S. Abdalla – kukagua Ujenzi wa Masoko Mkoa wa Mjini Magharibi
HabariHabari Mpya

Ziara ya Mhe. Hemed S. Abdalla – kukagua Ujenzi wa Masoko Mkoa wa Mjini Magharibi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla ameipa muda wa wiki mbili Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi na Baraza la Manispaa Magharibi B kukaa pamoja na mjenzi wa Soko la Mwanakwerekwe na Jumbi ili kupata ufumbuzi kuhusu ujenzi wa masoko hayo.

Makamu wa Pili wa Rais ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara yake kukagua kazi iliyofanywa kwenye miradi hiyo pamoja na Kituo cha Biashara Darajani.
Ameeleza wazi kwamba hajaridhishwa hata kidogo na hatua iliyofikiwa hadi sasa juu ya ujenzi wa masoko hayo, hivyo Serikali haioni kama mwekezaji huyo anaweza kukamilisha miradi hiyo kama ilivyotarajia.
Aidha amesema kwamba kutokana na hali aliyojionea, Serikali inapata mashaka juu ya uwezo wa kifedha wa mwekezaji huyo kuweza kufanikisha miradi hiyo miwili.

Makamu wa Pili wa Rais amesema pia ujenzi huo hauendi sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya Nane na kudai kuwa iwapo mwekezaji huyo ameshindwa kuendeleza ujenzi huo, Serikali itaangalia njia bora za kuendeleza miradi hiyo.

Vilevile ametoa indhari kwa wawekezaji kuwa wakweli pale wanapotaka kuwekeza katika miradi mbali mbali hapa nchini kwa vile azma ya Serikali ni kuona miradi hiyo inaleta manufaa kwa wananchi wake.
Wakati huo huo Mhe. Hemed ameipongeza Kampuni ya Africab inayojenga Kituo cha Biashara Darajani kwa kazi nzuri na inayoenda na wakati.
Ameieleza Kampuni hiyo kuwa Serikali itaendelea kuwapa mashirikiano ili kuhakikisha kuwa hakuna changamoto yeyote ile kwa upande wa Serikali na kuwataka watendaji wa Wizara, Mkoa na Manispaa kushirikiana na Kampuni hiyo ili iweze kutekeleza mradi huo kwa ufanisi.

Awali Viongozi wa Wizara, Mkoa na Manispaa walimuelezea Makamu wa Pili wa Rais kutoridhishwa kwao na kazi iliyofanywa hadi sasa na mwekezaji wa Soko la Mwanakwerekwe na Jumbi.
Ziara hiyo ya Makamu wa Pili wa Rais inafuatia ziara yake aliyoifanya kwenye miradi hiyo tarehe 15 Mei, ambapo aliahidi kurudi tena baada ya mwezi mmoja kuangalia hatua ya ujenzi iliyofikiwa.