OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC akutana na Tume ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai
HabariHabari Mpya

RC akutana na Tume ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai

Imeelezwa kuwa ipo haja kwa Serikali kutilia mkazo suala la maadili  kwa jamii ili kupunguza matendo yanayopelekea makosa ya jinai.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa na mazungumzo na Kamati ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mohamed Chande Othman.

Mkuu wa Mkoa amesema kutokana na ongezeko la makosa ya jinai, jamii hasa vijana wanahitaji kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya Kitanzania na Kizanzibari ili kuewaepusha na kuiga mambo ya nje ambayo yamekuwa yakiwaingiza katika makosa mbali mbali.   

Aidha amependekeza  pia  Serikali kujenga miundo  mbinu ya majengo   ya kisasa kwa taasisi zinazohusika na masuala ya haki jinai zikiwemo Mahkama na  vyuo vya mafunzo (Magereza), pamoja na kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara  wafanyakazi wa taasisi hizo.

Mkuu wa Mkoa aliishukuru Kamati hiyo kwa kufika katika Mkoa wake na kuweza kukusanya maoni ya wananchi wa makundi mbali mbali kwa azma ya kuboresha mfumo wa utendaji  kazi wa taasisi zinazosimamia haki jinai.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji Mkuu Msataafu wa Tanzania Mohamed Chande  Othman alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa mbali na kupokea maoni na mapendekezo ya wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi , tume itatembelea pia Chuo cha Mafunzo Kilimani na Chuo cha Polisi Ziwani  ili kujionea hali halisi ilivyo.