OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wafanyakazi wa umma watakiwa kuwa waadilifu
HabariHabari Mpya

Wafanyakazi wa umma watakiwa kuwa waadilifu

Wafanyakazi  wa  wizara, mashirika na taasisi mbali mbali wametakiwa kuwa waadilifu katika kusimamia mali za Serikali.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa wakati akifunga Semina ya siku tano kwa wahasibu, washika fedha, wahakiki mali na maafisa manunuzi  kuhusu usimamizi wa mali za Serikali iliyofanyika katika jengo la ZURA, Maisara.

Amesema kwamba upo mtindo kwa baadhi ya wafanyakazi wa kada hizo kufanya udanganyifu katika manunuzi na mauzo ya mali za umma kwa kutaka kujinufaisha wao binafsi na matokeo yake huitia hasara  Serikali.

Amewataka mafunzo waliyoyapata katika semina hiyo kwenda kuyatumia katika kutekeleza majukumu yao  sambamba na kufuata sheria na taratibu zinazowasimamia.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa  mali za Serikai ni mali za umma, hivyo wafanyakazi hao wanadhima kubwa ya kudhibiti mali hizo hatua ambayo itaisaidia Serikali kutumia fedha zake katika mambo mengine ya maendeleo.

Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Husseina Ali Mwiniyi kwa kuunda Ofisi ya Msajili wa Hazina na  Usimamizi wa Mali za Serikali  ambayo amesema itasaidia sana  kuhakikisha usalama wa mali za Serikali.

Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufunga Semina hiyo Msajili wa Hazina kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Wahid Mohammed Ibrahim Sanya amesema kumekuwepo na changamoto ya uharibifu wa mali  za  Serikali katika taasisi mbali mbali na kusema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu hao kusimamia kwa weledi mali za Serikali.

Nao  wafanyakazi walioshiriki semina hiyo wameahidi kuongeza juhudi katika kuhakikisha mali za umma zinasimamiwa ipasavyo.