OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Zoezi la kuwarejesha Wafanyabishara Darajani Souk laanza
HabariHabari Mpya

Zoezi la kuwarejesha Wafanyabishara Darajani Souk laanza

Uongozi wa Wilaya ya Mjini umeagizwa kusimamia zoezi la kuwarejesha wafanyabiashara waliyopo katika Skuli ya Darajani  kurudi kuendelea kufanya biashara zao katika kituo cha biashara cha Darajani Souk.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa wakati akizungumza na wafanyabiashara pamoja na uongozi wa Wilaya ya Mjini hapo Skuli ya Darajani kuhusiana na mpango wa kuhamia katika maduka mapya ya Darajani Souk.

Mkuu wa Mkoa ameagiza katika zoezi hilo kuhakikisha kuwa wafanyabiashara waliosajiliwa majina yao kabla ya ujenzi wa maduka wanapewa kipaumbele  cha kupatiwa milango katika eneo hilo la Darajani Souk ili waweze kuendelea na biashara zao.

Aidha Mhe. Idrissa amewataka wafanyabiashara wa  hao kufuata utaratibu wa kuweka bidhaa zao kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa  kwa kila maduka ili kuwarahisishia wateja kununua bidhaa wanazohitaji.

Vilevile Mkuu wa Mkoa amewaasa wafanyabiashara hao wayatunze maduka waliyokabidhiwa na waache utamaduni wa kuweka bidhaa nje ya maduka ili kuepusha usumbufu kwa watu watakaofata huduma kwenye eneo hilo.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mhe. Rashid Simai Msaraka amesema kuwa tayari wameanza kulifanyia kazi agizo hilo la Mkuu wa Mkoa kwa kuanza na wafanyabiashara wa vitambaa  kurudi katika eneo hilo.

Naye mmoja ya wafanyabiashara hao, Juma Mohammed Naftal ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwawekea mazingira mazuri na salama katika kufanya biashara zao na kuiomba kuangalia suala la kodi ili lisiwe kikwazo kwa wafanyabiashara kumudu kukodi milango hiyo.