OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC afunga Mkutano wa TAUTA
HabariHabari Mpya

RC afunga Mkutano wa TAUTA

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa ameitaka Jumuia ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa (TAUTA), kukitumia chombo hicho kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuuenzi na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa TAUTA  uliyofanyika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani, Idrissa amesema mbali na majukumu mengine ya Jumuia hiyo, TAUTA itaweza kuwa mabalozi wazuri wa kuutetea Muungano kutokana na uzalendo na uadilifu mkubwa waliyoonesha wanachama wake katika kulitumikia taifa.

Mkuu wa Mkoa amewapongeza kwa kuunda Jumuia hiyo ambayo amesema itawaunganisha wakimbiza Mwenge wa Uhutu Kitaifa kutoka Mikoa yote ya Tanzania.

Kwa upande mwengine Idrissa  amesema  iwapo mpango mkakati  wa  miaka mitano waliyoupitisha kwenye mkutano huo watautekeleza ipasavyo Jumuia hiyo itaweza  kupata maendeleo na mafanikio makubwa ndani ya kipindi hicho. 

Aidha amewashauri kuwa na miradi ya kiuchumi ambayo itaenda sambamba na mipango ya Serikali ikiwemo  uchumi wa buluu, uvuvi na kilimo na kusema kuwa Serikali ya Mkoa wake itakuwa tayari kuwapa kila aina ya mashirikiano katika kufanikisha miradi hiyo. 

Nae Mwenyekiti wa TAUTA Mhandisi Charles Kabeho amesema kwamba bado wanaendelea na juhudi za kuwaunganisha wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kote nchini ili waweze kutekeleza malengo yao kwa ufanisi zaidi.

Amesema mbali na mkutano huo vievile watashiriki katika zoezi la upandaji miti  ili kuunga mkono ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2023 kuhusu uhifadhi wa mazingira sambamba na kuzuru kaburi la Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara na Zanzibar akiwemo Kepteni  Mstaafu Mzee Daniel Paul  Assey aliyekimbiza Mwenge wa Uhuru wa kwanza mwaka 1964.