OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Kitwana awahimiza madereva wa bodaboda kuvaa sare.
HabariHabari Mpya

Kitwana awahimiza madereva wa bodaboda kuvaa sare.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amewahimiza madereva wa Boda boda  kuhakikisha wanavaa  sare na beji  zitakazowatambulisha ili watumiaji wa usafiri huo waweze kuwatambua madereva waliosajiliwa  kuifanya kazi hiyo.

Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo katika kikao chake na  Uongozi wa Jumuia ya Waendesha Bodaboda hapo Afisini kwake Vuga.

Amesema kutokana na ongezeko la vyombo hivyo kuna umuhimu mkubwa wa madereva hao kuvaa sare pamoja na beji ili jamii iweze kuwatambua na kuhakikisha  usalama wao pale wanapotumia usafiri huo.

Aidha amesema amewataka madereva wa bada boda kufuata sheria na taratibu zilizopo kwani takwimu zinaonesha idadi kubwa ya ajali na vitendo vya kihalifu vinatokana  madereva wa vyombo hivyo.

Katika kudhibiti vitendo hivyo Mkuu wa Mkoa amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa Mjini Magharibi  kuendesha operesheni za mara kwa mara za kuwakamata madereva wanaoendesha vyombo hivyo bila leseni na  wanaovunja sheria za barabarani.

Kwa upande  mwengine  Idrissa ameutaka uongozi wa madereva  wa boda boda kuwashajiisha wanachama wao kujiunga na mafunzo yanayotolewa na Idara ya Mawasiliano kwa madereva wa boda boda.

Amefahamisha kuwa Serikali imepunguza malipo ya mafunzo hayo kutoka shilingi laki mbili hadi elfu arubaini kwa lengo la kutaka madereva wote kupata  mafunzo hayo na kuwataka kuitumia vizuri fursa hiyo.

Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa Serikali imerasimisha vyombo hivyo kuwa usafiri rasmi wa kubeba abiria, hivyo kuna umuhimu wa kupata mafunzo hayo ili waweza kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Kadhalika amewashauri  kuwa na siku maalumu itakayowakutanisha madereva hao  kwa lengo la kuzungumzia changamoto zinazowakabili, mafanikio yao pamoja na njia za kuboresha usafiri huo.  

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi  Richard Mchomvu ameahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Mkuu wa Mkoa na kuwataka madereva wa boda boda kufuata sheria ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Uongozi wa Jumuiya ya Madereva wa Bodaboda wameiomba Serikali ya Mkoa kuwathibiti waendesha boda boda wasiyosajiliwa kwa vile wamekuwa wakiichafua kazi hyo na kujihusidha na matendo ya uhalifu.

Kati ya boba boda 2119 zilizosajiliwa, madereva 911 sawa na asilimia 4.6 ndio waliokiswapata mafunzo kufanya kazi hiyo.