Serikali ya Mapindunzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuimarisha miundombinu rafiki kwa vijana ili kuwawezesha kujiajiri kwa kuendelea kujenga vyuo vya mafunzo ya amali mbali mbali kwa ajili ya kuwapatia vijana ujuzi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Mohammed Mussa wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Mafunzo kwa vijana kilichopo Bweleo Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni shamra shamra ya kuelekea mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa ni vyema kwa vijana wa Wilaya mbali mbali za Zanzibar kuitumia fursa hiyo ya kuanzishwa kwa kituo hicho kwani kutaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na tatizo la ajira. Akielezea Mapinduzi matukufu ya Zanzibar Mhe Leila amesema vijana wengi wamekuwa wakiyasoma kupitia historia ya Mapinduzi ya Zanzibar hivyo wanawajibu mkubwa ya kuyaenzi kwani lengo la wazee kufanya mapinduzi ni kuondoa madhila ambayo yalikuwa yakifanyika kutoka kwa watawala kwa wakaazi wa visiwa vya Zanzibar.
Akitoa Salamu za Mkoa wa Mjini Magharibi Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mhe. Hamida Mussa Khamis amesema Mkoa huo utaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika kuhakikisha vijana wa Wilaya zote za Mkoa wa Mjini Magharibi wanazitumia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo mafunzo mbalimbali.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi Fatma Hamad Rajab amesema awali eneo hilo lilikuwa likitumika kwa matumizi mengine na ndipo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipowalipa fidia wananchi ili kuweza kuanzisha kituo cha kuwapatia Mafunzo Vijana .
Zaidi ya Shilingi Milioni mia mbili zimetumika kufanyiwa ukarabati jengo hilo ambazo zote zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.