OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>SMZ yaimarisha miundombinu kwa vijana kuweza kujiajiri
HabariHabari Mpya

SMZ yaimarisha miundombinu kwa vijana kuweza kujiajiri

Serikali ya Mapindunzi ya Zanzibar imesema itaendelea  kuimarisha miundombinu rafiki kwa vijana ili kuwawezesha  kujiajiri kwa kuendelea kujenga vyuo vya mafunzo ya amali mbali mbali kwa ajili ya kuwapatia vijana  ujuzi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Mohammed Mussa wakati wa ufunguzi wa  Kituo cha Mafunzo kwa vijana kilichopo Bweleo Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi,  ikiwa ni shamra shamra ya kuelekea mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa ni vyema kwa vijana wa Wilaya mbali mbali za Zanzibar kuitumia fursa hiyo  ya kuanzishwa kwa kituo  hicho kwani kutaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na tatizo la ajira. Akielezea Mapinduzi matukufu ya Zanzibar  Mhe Leila amesema vijana wengi wamekuwa wakiyasoma  kupitia historia ya Mapinduzi ya Zanzibar  hivyo wanawajibu mkubwa ya kuyaenzi kwani lengo la wazee kufanya mapinduzi ni kuondoa madhila ambayo yalikuwa yakifanyika kutoka kwa watawala kwa wakaazi wa visiwa vya Zanzibar.

Akitoa Salamu za Mkoa wa Mjini Magharibi Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mhe. Hamida Mussa Khamis amesema Mkoa huo utaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika kuhakikisha vijana wa Wilaya zote za Mkoa wa Mjini Magharibi  wanazitumia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo mafunzo mbalimbali.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi Fatma Hamad Rajab amesema awali eneo hilo lilikuwa likitumika kwa matumizi mengine na ndipo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipowalipa fidia wananchi ili kuweza kuanzisha kituo cha kuwapatia Mafunzo Vijana .

Zaidi  ya Shilingi Milioni mia mbili  zimetumika kufanyiwa ukarabati   jengo hilo ambazo zote zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.