OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Rc Kitwana awataka watendaji kushiriki ziara ya Rais Mwinyi
HabariHabari Mpya

Rc Kitwana awataka watendaji kushiriki ziara ya Rais Mwinyi

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewataka watendaji na maofisa wa Serikali wanaosimamia ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo kushiriki kikamilifu katika ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi itakayoanza tarehe 16 hadi 18 mwezi huu katika Mkoa huo.

Wito huo ameutoa hapo Afisi ya Mkuu wa Mkoa Vuga wakati akitoa taarifa kuhusu ziara hiyo ndani ya Wilaya tatu za  Mkoa wake.

Amesema mbali na ushiriki wao watendaji hao ni muhimu kuchukua nyaraka zote zinazohusu miradi itakayokaguliwa na Rais wa Zanzibar kwenye ziara hiyo ili waweze kutoa ufafanuzi sahihi pale watakapotakiwa kufanya hivyo.

Mkuu wa Mkoa ameitaja  miradi  itakayotembelewa ni pamoja na ujenzi wa miradi ya sekta ya  maji, barabara, elimu, afya, wajasiriamali, michezo na miradi ya  wananchi na wawekezaji ambayo baadhi yake itawekewa mawe ya msingi na iliyokamilika itazinduliwa rasmi.

Amesema katika miradi hiyo imo inayojengwa kupitia fedha za UVIKO 19, mkopo wa Benki ya Exim ya India pamoja na miradi inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Wawekezaji.

Aidha Idrissa amefafanua kuwa ziara hiyo itaanza kwa Rais wa Zanzibar kupokea Ripoti ya Utekelezaji wa Shuguli za  Maendeleo kwa Mkoa Mjini Magharibi katika mkutano utakaofanyika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi na kumalizia siku ya mwisho kwa mkutano wa majumuisho utakaofanyika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kiwakujuni  ambapo Viongozi na Watendaji wa Sekta zote wametakiwa kuhudhuria.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi amewahimiza  wananchi wa Mkoa wake kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo yote yenye miradi itakayotembelewa na Rais wa Zanzibar kwa lengo la kumuunga mkono jitihada zake anazochukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa huo na Zanzibar kwa ujumla.

Amesema akiwa katika ziara hiyo mbali na kukagua miradi, Rais wa Zanzibar atatumia fursa hiyo kusalimiana na wananchi na kuwasikiliza changamoto zao ili Serikali yao sikivu  iweze kuzipatia ufumbuzi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Husein Ali Mwinyi ataanza ziara yake Mkoa Mjini Magharibi katika Wilaya ya Magharibi A, siku ya pili  Wilaya ya Magharibi B na kukamilisha siku ya tatu Wilaya ya Mjini.