OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Zitumieni vyema fursa za mikopo – RAS
HabariHabari Mpya

Zitumieni vyema fursa za mikopo – RAS

Vikundi vya wajasiriamali na wavuvi waliopatiwa mikopo kupitia fedha za UVIKO 19 wametakiwa kuitumia vyema fursa ya mikopo  waliyoipata katika kuendeleza kazi zao pamoja na kujipatia kipato.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala  Mkoa Mjini Magharibi Mohamed Ali Abdallah katika kikao na Vikundi vya wavuvi pamoja na watendaji wa Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Vuga.

Amesema licha ya mikopo hiyo isiyo na riba kuanza kuwanufaisha baadhi ya wajasiriamali na vikund vya wavuvi, hata hivyo bado kuna haja ya kuwaelimisha walengwa ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Akizungumzia changamoto zilizojitokeza kwa vikundi vya wavuvi, Katibu Tawala amevitaka vikundi hivyo kuwa wastahamilivu huku Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu ikizitafutia ufumbuzi wa haraka changamoto hizo.

Kwa upande wao vikundi vilivyopata  boti za uvuvi wameeleza kuwa bado kuna vifaa muhimu walivyoahidiwa hawajapatiwa na hivyo kushindwa kuzitumia boti hizo vilivyo kwa ajili ya kazi zao.

Aidha wameomba kupunguziwa kiwango cha fedha wanachotakiwa kurudisha benki kila mwezi kwa kuwa kiwango hicho hawakimudu kutokana na kipato wanachoingiza.

Nae Mkurugenzi Uendeshaji Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu Issa Suleiman Ali   amesema Wizara yake imepokea changamoto na maombi yalitolewa na vikundi hivyo na watakaa na wadau husika ili kuangalia namna ya kuyapatia ufumbuzi.