OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mbio za Mwenge wa Uhuru zaridhishwa na ujenzi wa mradi wa maji.
HabariHabari Mpya

Mbio za Mwenge wa Uhuru zaridhishwa na ujenzi wa mradi wa maji.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongewa kwa ujenzi wa miradi mikubwa ya Maendeleo katika Mkoa Mjini Magharibi.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa matangi ya maji  huko Kama, Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru 2023 Abdallah Shaib Kaimu  ameeleza kuridhishwa na kazi iliyofanywa katika mradi huo.

Ameitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha miradi hiyo inajengwa katika kiwango kinachotakiwa na kukamilika kwa wakati.

Ameongeza  kwa kusema kwamba  miradi hiyo inatumia fedha nyingi za Serikali hivyo ni muhimu kuona inaleta manufaa kwa wananchi kama  ilivyokusudiwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Suzan P. Kunambi ameahidi kuwa wataendelea kufuatilia ujenzi wa miradi kwenye Wilaya yake na hatosita kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi watakaojenga chini ya kiwango.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Mhe. Machano Othman Said ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa  na kusema unakwenda kuondosha tatizo la maji kwa wananchi wa Jimbo lake.

Akiwa katika mradi huo Kiongozi pamoja  na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa walikagua ujenzi  sambamba na kupitia nyaraka zake mbali mbali  kabla ya kuweka jiwe la msingi.